Recent

JIFUNZE MAMBO MBALIMBALI YATAKAYOKUPA MAARIFA NA UJUZI MAISHANI

Wednesday, 31 August 2016

WARAKA WANGU KWA MARAIS WASTAAFU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.NDUGU ALI HASSAN MWINYI, BENJAMINI WILLIAMU MKAPA NA JAKAYA MRISHO KIKWETE.

Awali ya yote nawasalimia wazee wetu,salaam!
Ninayo furaha kuandika waraka huu kwenu wazee wetu ambao kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mmeweza kuwepo mpaka leo toka mstaafu katika kuiongoza nchi yetu ya Tanzania.Hongereni sana!
      
                Lengo kuu la kuandika waraka huu kwenu ni juu ya nia yangu ya dhati niliyonayo juu ya Taifa letu, kuona sisi kama Taifa tunaendelea kuwa taifa la amani na ustawi katika kujiletea maendeleo yaliyokusudiwa na mwasisi wa taifa hili Mwl J.K Nyerere baada wa ukombozi kutoka mikononi mwa mkoloni.Na hii imetokana na mvutano uliopo sasa kati ya serikali na vyama vya upinzani juu ya mikutano ya kisiasa.Pili nimeona nitumie nafasi hii,kuweza kuwaomba ninyi kama walezi na wazee wetu wazoefu na nchi hii kuingilia kati jambo kubwa namna hii ambalo linaweza kuiweka nchi mahali ambapo sura yake ya zaidi ya miaka 50 ya uhuru itachafuka ndani ya muda mfupi, ndani na nje ya nchi.Waswahili husema palipo na wazee huwa hapaharibiki jambo,na uzee ni jalala ndiyo maana nawatupia jambo hili mlitazame kama wazee wazoefu na siasa za nchi hii.

       Kwanini nimeandika waraka huu kwenu wala si kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ndugu Josephu John Pombe Magufuli,nimeandika kwenu kwa sababu moja tu kubwa ,kwakuwa mvutano huu unapande mbili hakika usuruhishi wake hauwezi kupatikana miongoni mwa pande hizo mbili bali usuruhishi wake unapaswa kutoka kwa mtu wa tatu ambaye atasikiliza maoni ya pande zote mbili,ili kujua nani yuko sahihi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,sina maana kuwa pande zote mbili hazijui sheria bali kwakuwa zote zinavutana basi mvutano huo unaweza pia ukaziba macho yao yasione nani mwenye haki kisheria.

          Lakini pia kwakuwa ninyi wazee wetu mpo bado angali hai,ni lazima tuwatumie wakati mwingine kutatua mambo mazito kama haya,haiwezekani mambo yaharibike tuanze kuwalaumu kwamba mpaka mambo yanaharibika hivi hawa
wazee hawakuwapo? Na kwa jinsi hiyo pia tunakuwa tumetambua umuhimu wa uwepo wenu kama walezi wa taifa.

    Wako watu katika taifa hili mimi nikiwa mmoja wapo ambao wanatamani uwepo wa wazazi wao ili waweze angarau kuwashauri wanapokumbana na changamoto ngumu katika maisha, lakini wazazi hao hawapo,sasa sisi kama taifa bado tunakila sababu ya kujivuna kuwa na wazazi wetu ambao kazi kubwa iliyo baki kwenu nikutoa ushauri kwa vijana wenu ili mambo yakae vema na heshima ya nchi yetu iendelee kutamalaki.
   
Tumesikia kauli mbali mbali zikitolewa pande zote upande wa serikali na upande wa upinzani,kauli ambazo ukizipima zinaashiria shari na sio amani,sasa sisi kama wananchi wa kawaida ambao tumekulia katika nchi ya kistaarabu tunapata shida na kauli hizi kwamba malengo yake ni nini,watanzania tunasifika duniani kwa uungwa,utu na ustaarabu wa hali ya juu zaidi kauli hizi zinazotoka pande zote zinatufanya tupate shida ya kutafsiri aina ya utu tulio nao leo,kwahiyo ndio maana nikaona niwaombe ninyi wazee wetu mlitazame jambo hili kama linazungumzika.

        Mfalme sulemani alimwomba Mungu ampatie mambo mawili tu nayo ni Hekima na Busara,naamini mambo hayo mawili ninyi mnayo ndiyo maana mliweza kuiongoza nchi hii na leo tunawaheshimu kama wazee wetu.Jambo hili si la kukaa kimya,inawezekana hamjakaa kimya mmekuwa mkifanya juhudi za kuhakikisha yale yanayotarajiwa kutokea yasitokee,lakini mimi kama kijana ninayelitazama taifa hili kwa umri wangu sasa natimiza miaka 29 tangu nijitambue skuwahi kuona kauli za namna hii ambazo zinatamkwa sasa.
    
       Ndugu Jakaya mrisho kikwete,mwaka jana nilikwandikia barua ya wazi iliyo toka katika gazeti la Nipashe la tarehe 20 october 2015 ukurasa wa 7 yenye kichwa cha habari BARUA YA WAZI WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA JK.

      Barua hiyo pia ilirudiwa katika gazeti la Mwanahalisi la tarehe 26,katika barua ile nilionyesha wazi mambo makubwa na mazuri uliyoyafanya katika uongozi wako,miongoni mwa hayo ilikuwa ni Jambo la barabara,Ujenzi wa shule za kata ambazo kimsingi ndizo shule za kwanza kujengwa na serikali ya Tanzania na mwisho nilieleza namna ambavyo ulikuza Demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na wananchi wa nchi hii kuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza hilo nilikusifu sana na nikasema utakapomaliza muda wako kama Rais wa Tanzania hautakuwa Rais mstaafu tu wa Tanzania bali utakuwa kiongozi wa kimataifa na bado naamini ipo siku utakuwa kiongozi mkubwa sana  wa kimataifa.Hii ni kutokana na demokrasia uliyoijenga kwa kipindi chako,inawezekana wapo watu walinishangaa kwa wakati huo lakini niliona dhamira yako ya dhati ya kutohitaji kutenda maouvu juu ya wananchi wako.

            Nichukue nafasi hii tena nikuombe wewe pamoja na marais niliowataja hapo juu kulitazama suala hili ambalo linatishia amani ya nchi yetu na mimi naamini siku zote meza ya mazungumzo ndio huwa dawa katika migogoro yote,polisi,jeshi wala mahakama huwa si suruhisho lenye kuleta mapatano bali mapatano ya kweli hupatikana mezani ambapo pande mbili hukutanishwa na mtu wa tatu.
 Tanzania ni nchi inayotazamwa na nchi karibu zote Afrika na duniani kama mfano wa amani na uhuru wa watu wake,itakuwa aibu kubwa nchi kuingia kwenye machafuko tufanane na majirani zetu najiuliza kama tukiyaacha haya yakatimia ni nani atakuwa mshauri wa mwenzake? Ni waombe sana wazee wetu bado sisi kama vijana tutapenda kuona tunaishi kwa amani, amani ambayo itatokana na misingi ya Katiba na sheria za nchi tulizojiwekea.

          Ningeamua kunyamaza kimya lakini roho yangu hainitumi naona ninalo jambo la kuwaelezeni ninyi ili kwa pamoja tuendelee kuifurahia nchi hii kama mlivyoweza kuifurahia ninyi na leo mnaitwa viongozi wastaafu.
     Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema maneno haya “Demokrasia haiwezi kudumu ikiwa wachache hawatakubali matakwa ya wengi.Lakini matakwa ya wengi hujurikana katika majadiliano au mazungumzo ya waziwazi. Kadhalika, matakwa ya wachache hujulikana katika majadiliano na mazungumzo bila wale wachache kusema waziwazi matakwa yao ,majadiliano hayana maana” Nyerere J.K (1962) Tujisahihishe.

       Hapa mwalimu pamoja na mambo mengine msisitizo mkubwa hapa ni juu ya majadiliano ambayo yanapaswa kutoka pande mbili ambazo zinavutana na ndiyo maana nikaona ni busara mazungumzo hayo yawe na mtu wa tatu atakaye sikiliza hoja za pande zote na kuhakikisha muafaka unapatikana na kila mtu analizika na uamzi wa majadiliano hayo.
            
      Mimi si mwanasheria kwahiyo siwezi kusema nani mwenye haki kati ya serikali na vyama vya upinzani,pia siwezi kusema nani asiye na haki katika kutekeleza shughuli zake, wote wanaweza kuwa sahihi na wote wanaweza wasiwe sahihi lakini usahihi huo ndio unapaswa kujengwa kwa hoja mbele yenu ili mfikie muafaka mzuri bila kurushiana maneno,lazima tutambue kuwa sisi sote ni watanzania na nchi hii ni ya kila mtu,akuna aliyemleta mwenzake duniani akamwambia wewe utaishi Tanzania bali wote tumezaliwa katika ardhi hii ya Tanzania hivyo majadiliano mbele yenu ni muhimu sana.
     
    Silaha za kivita marazote huwa hazileti amani,bali machafuko. Sisi wote ni mashuhuda wa nchi ambazo wamekuwa katika migogoro ya kisiasa, lakini kinachowafikisha huko nikutokuwepo majadiliano au mazungumzo yenye maelewano na athari zake si kwa yule tu aliyekusudiwa hata yule aliyekusudia kufanya hivyo hupata athari,hivyo kwa mtazamo wangu ni muhimu sana wazee wetu,viongozi wetu jambo hili mlitazame kabla hatujashudia yale wengi wanaodhani yanaweza kutokea ili yaishe kwa amani na tuendelee kuwa waalimu wa Amani Afrika na Duniani kote.

           Mwisho,naamini  bado sisi watanzania ni wamoja  kwakuwa sisi sote ni ndugu na haya ndiyo matunda aliyotuachia baba wa taifa letu Mwl J.K Nyerere hatubaguani kwa misingi ya dini,kabila,rangi,au vyama vya siasa.Kama dalili za mambo haya zitaanza kuonekana ni lazima tujiuleze ni kweli tutakuwa tunamuenzi mwl mtu ambaye ametufanya leo tunajiona watanzania au tutakuwa wasalti wa fikra hizo?
Niwatakie mafanikio mema katika mjadala huo ambao utatoa wingu zito lililotanda katika anga la Tanzania huku tukiona maandalizi ya pande zote yakiendelea, sijakamilika mtanisamehe pale nitakapokuwa nimewakwaza.

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA.
           
Magabilo Masambu(29)
           
0758379296,0717735023.

0 comments:

Post a Comment