Thursday, 18 August 2016
Usichokijua kuhusu Yusuf Manji
Kwanza kabisa fahamu kwamba Yusuf Manji alichaguliwa na wanayanga mwaka 2012, Yanga ikiwa haifanyi vizuri katika mpira ukilinganisha na wahasimu wake Simba. Baada tu ya Yusuf Manji kuingia madarakani, mwaka 2012 Yanga ikatwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Tokea kipindi hicho hadi sasa Yanga imeshatwaa ubingwa mara 3.
Hivi karibuni watu wamezua sintofahamu juu ya adhma ya Yusuf Manji Jangwani. Nia na madhumuni ya Manji kwa Yanga ni kuwekeza ili klabu iwe na uwezo mkubwa zaidi na siku moja iweze kushindana kimataifa na hata iweze kutwaa ubingwa wa Afrika.
Kuna mambo mengi ambayo watu wengi hawajui kuhusu Yusuf Manji. Yeye kama Mwenyekiti ndiye aliyependekeza na kuwezesha kupandishwa mishahara kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi iliosababisha kwa namna moja au nyingine kuleta mafanikio ya Yanga tunayoiona leo.
Fahamu kwamba mkataba kati ya TBL na Yanga ulipokwisha muda wake mwaka huu, hakuna hata kampuni moja iliyojitokeza kwa ajili ya udhamini mpya. Manji kwa mapenzi yake akaona aende kuiombea Yanga udhamini kutoka katika kampuni ambayo alishawahi kuwa mwenyekiti wake.
Kwa kuangalia yote ambayo Manji ameyafanya kwa kujitoa kwa hali na mali, inashangaza kwamba mtu anaweza simama akasema kwamba kuna dalili za rushwa wakati hata huko nyuma, Manji alifanya mambo yote kwa uwazi kabisa. Tujiulize, ufisadi ni kutoa au kuchukua hela? Na je Manji amekuwa akitoa au kuchukua hela Yanga?
Kwa mapenzi yake kwa klabu pamoja na mpira wa Kitanzania, Manji amekua akichangia kwa kiasi kikubwa lakini leo watu ambao hatujawahi kuwasikia wakichangia lolote kwenye mpira wanapaza sauti na kuleta kashfa zisizokuwa na ushahidi wowote. Wanamichezo wenzangu pamoja na wapenzi wote wa mpira, tuwakatae watu wa haina hii kwa nguvu zote.
Mafanikio waliyoyapata Yanga ndani ya kipindi ambacho Manji amekuwa mwenyekiti sio yakuyabeza hata kidogo, tukifanya mchezo tunaweza rudi kule tulipotoka. Si unajua msemo wa adui yako muombee njaa? Ndio wanachotuombea watani wetu.
Mwezi Julai 2016 Yusuf Manji alichaguliwa na wanachama wa Yanga kwa asilimia 100 kuwa mwenyekiti kwa kipindi cha pili mfululizo. Hii inadhihirisha ni jinsi gani wanachama wa Yanga walivyo bado na imani na mwenyekiti wao.
Watu watambue kwamba Manji hajaanza kujihusisha au kuichangia Yanga mwaka 2012 pindi alipoutwaa uwenyekiti bali alianza kipindi cha nyuma zaidi na Yanga imekua ikinufaika kwa miaka mingi sana.
Ukiachana na mpira Yusuf Manji pia amekua na mchango mkubwa sana hapa Tanzania. Kupitia makampuni yake ameweza kuwapatia ajira Watanzania wengi sana. Licha ya hayo yote, pale anapojaribu kuwekeza upande wa pili wa michezo watu wanaleta hoja za kumpinga na kutaka kudhoofisha azma yake ya kutaka kuleta mabadiliko yenye tija.
Yusuf Manji amekuwa ni mwanzilishi wa “Africa Against Ebola Solidarity Trustee“ ambayo ilikua chini ya uangalizi wa Thabo Mbeki ilyokuwa na lengo la kutokomeza Ebola barani Afrika. Manji ameweza kusimamia na kufanikisha uchangishwaji wa mamilioni ya pesa na yeye akiwa mmoja kati ya wachangiaji wakubwa katika mfuko huo. Hata baada ya kufanya yote hayo, Manji hajawahi kujitangaza kwa hayo yote ambayo ameyafanya.
Dunia imekuwa ikitambua michango ya Yusuf Manji na hadi kumpa tuzo mbalimbali. Mfano, mwaka 2015 alipewa tuzo ya Iconic business leader of the year ambayo pia alishawahi kupewa pia Sheikh Ahmed Bin Saeed Maktoum, Chairman and CEO of Emirates na watu wengine wengi maarufu.
Katika siasa aliamua kuingia katika kinyanganyiro cha udiwani ambao watu wengi walidhania ni cheo kidogo kwa mtu mwenye wadhifa wake lakini alifanya hivyo ili kuweza kuwafikia zaidi watu kwa ukaribu. Amekua akichangia sana katika sekta ya Elimu Mbagala Kuu. Licha ya haya yote anayofanya bado kuna watu wanaamua kumvunja moyo kwa kupinga mipango ambayo anataka kuendelea kuitekeleza kwa ajili ya jamii ya Tanzania.
Yusuf ambae amekaririwa na Saleh Jembe Blog kuwa “wamuache amechoka” ni kuonyesha kuwa yeye pia ni binadamu na anaumia kama wanavyoumia binadamu wengine.
Pale mtu anapoamua kuchangia pesa zake binafsi kwa ajili ya jambo jema,hatuna budi wananchi pamoja na viongozi kumtia moyo na kumpa ushirikiano ili azma iweze kufikiwa. Yusuf Manji hajawahi kuchukua kitu chochote Yanga wala hajawai kuomba kitu kutoka kwa Yanga au wanachama wake zaidi ya ushirikiano.
Hatuna budi kumwachia Manji akaendelea kuiboresha timu yetu iwe ya kimataifa zaidi na kutufanya wana Yanga tuendelee kufurahia ushindi na wapenzi wa mpira nchini wakijionea Yanga inavyosonga mbele. Maana nyuma sie kwetu mwiko.
0 comments:
Post a Comment