Thursday, 4 August 2016
Je wajua? Shushushu (Afisa Usalama wa Taifa) ni mtu wa aina gani, anafanya nini?
PART 1
Kuna ukweli mmoja usiofichika wala kupingika kwamba watu wengi sana wanapenda kazi ya ushushushu, yaani Uafisa Usalama wa Taifa.Hiyo sio kwa Tanzania pekee bali sehemu nyingi duniani. Ukiingia mtandaoni utakutana na watu wengi wanaozungumzia taaluma ya intelijensia au/na wahusika katika hali ya kutamani kuifahamu taaluma hiyo nyeti au kuwa mhusika.
Leo nitaanza mlolongo (series) wa makala kuhusu taaluma hiyo adimu. Hata hivyo ni vema nikatahadharisha mapema kwamba nitakachoandika ni kile tu kinachoruhusiwa kuandikwa hadharani. Kimsingi,taaluma ya ushushushu inatawaliwa na usiri,na mengi ya yanayohusiana na taaluma hayo yanabaki kuwa siri. Hata hivyo,kuna maelezo ambayo yapo wazi japo inahitaji uelewa wa aina flani kuchora mstari kati ya kipi ni siri na kipi ni ruksa kuwa hadharani.
Kwa tafsiri rahisi, ushushushu ni taaluma inayohusu ukusanyaji wa taarifa za kiusalama kwa njia za siri (clandestine methods). Japo kwa kiswahili ushushushu ni intelijensia, kiundani kuna tofauti kati ya ushushushu unaofanyika ndani ya nchi na unaofanyika nje ya nchi.Kwa hapa Uingereza, Idara ya ushushushu inayoshughulika na masuala ya ndani inajulikana kama MI5 na inayohusiska na ushushus nje ya nchi ni MI6.Kwa huko nyumbani, tofauti hizo zipo ndani ya muundo wa taasisi husika, kwa maana kwamba kuna taasisi moja tu lakini ndani yake kuna mgawanyo wa kimajukumu ya ndani na ya nje.
Kadhalika, japo mashushushu wamekuwa wakifahamika pia kama spies, ukweli ni kwamba spy ni shushushu anayefanya kazi nje ya nchi yake,kitu kinachojulikana kiusalama kama ujasusi au espionage kwa Kiingireza.
Japo mataifa mbalimbali yana miundo tofauti ya Idara zao za Usalama wa Taifa,lengo na kazi kuu ni ukusanyaji wa taarifa hizo.Kwa minajili ya makala hizi, nitazungumzia zaidi mazingira ya huko nyumbani Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1996, Idara yetu ya Usalama wa Taifa ni idara ya serikali iliyo chini ya Ofisi ya Rais,ambayo ina jukumu la kukusanya na kuchambua taarifa za usalama na kuziwasilisha 'mahala kunakohusika' katika namna ambayo Mkurugenzi Mkuu wa Idara hiyo ataona inafaa.
Kimsingi, mkuu'halisi' wa Idara hiyo ni Rais mwenyewe,ambaye kwa lugha ya kiusalama anafahamika kama 'sponsor.' Wakuu wa Idara za usalama popote pale duniani hufahamika kama spymaster.
Maeneo makuu ya kazi za Idara ya Usalama wa Taifa ni kukusanya na kuchambua habari za kiusalama zinazohusiana na ujasusi (espionage),uzandiki (subversion),uhujumu (sabotage) na ugaidi (terrorism). Lakini jukumu la Idara hiyo si kukusanya taarifa hizo na kuzichambua tu bali pia kuzuwia matukio hayo yanayofahamika kama matishio ya usalama wa taifa.
Ni kwa vile utendaji wa kazi wa Idara yoyote ile ya Usalama wa Taifa unaegemea katika usiri mkubwa ndio maana kwa 'mtaani' kuna hisia tofauti kuhusu umuhimu wa taasisi hiyo. Ukweli ni kwamba laiti umma ungefahamu nini kinafanywa (au kinapaswa kufanywa) na Idara hiyo basi kwa hakika ingethaminiwa zaidi ya kuogopwa tu. Ni muhimu hapa nisisitize kuwa ninazungumzia 'hali mwafaka' yaani kwa Kiingereza ideal situation. Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko mengi miongoni mwa wananchi wakiishutumu Idara yetu ya Usalama wa Taifa kuwa imeleemea mno kwenye siasa hasa kuibeba CCM,imezembea mno kiasi cha kuruhusu ufisadi kushamiri, na imekuwa ikilaumiwa pia kutokana na matukio mbalimbali yanayotishia usalama wa Taifa kama vile ugaidi.
Wanaotoa lawama hizo wapo sahihi kwa kiasi flani,kwani kushamiri kwa maovu katika jamii sambamba na mwendelezo wa matukio yanayotishia usalama wa taifa ni viashiria kuwa Idara ya Usalama ya nchi husika ina mapungufu kiutendaji.
Hata hivyo,ni muhimu kutambua kanuni moja muhimu ya ufanisi au kushindwa kimajukumu kwa Idara ya Usalama wa Taifa popote pale.Ni kwamba wakati Idara husika inapaswa kuwa macho katika kila sekunde kuzuwia matendo ya kidhalimu, wanaopanga kufanya matendo hayo wanahitaji mara moja tu kufanikisha azma yao.Mfano halisi ni kwenye matukio ya ugaidi. Wakati gaidi anahitaji fursa moja tu kufanikisha tukio la kigaidi, Idara ya Usalama inahitaji kila fursa- kila sekunde,dakika,saa,siku,wiki,mwezi,mwaka-kuhakikisha gaidi hafanikiwi.
Kadhalika, wakati inaweza kuwa rahisi kuilaumu Idara ya Usalama wa Taifa inaposhindwa kuzuwia tukio flani, kwa mfano shambulio la kigaidi nchini Kenya, kiuhalisi suala zima la ukusanyaji wa taarifa za kiusalama ni gumu mno. Hebu pata picha: unaletewa tetesi kuwa kuna mtu anataka kulipua bomu kanisa au msikiti. Mara nyingi tetesi hizo huwa hazibainishi jinsia ya mtu huyo,wajihi wake,ni mwenyeji au mgeni na vitu vingine muhimu vya kuweza kumtambua japo kwa ugumu.
Kutokana na ugumu wa zoezi la kukusanya taarifa za kiusalama,ndio maana wahusika-mashushushu/maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa-wanapaswa kuwa watu wenye akili isiyo ya kawaida, au angalau wenye uwezo mkubwa wa kutumia akili.Neno lenyewe intelijensia linahusiana na matumizi ya akili.Lakini si akili tu, bali pia maafisa usalama wa taifa hupaswa kujifunza na kuendeleza hisia ya sita (6th sense). Mwanadamu wa kawaida ana hisia 5: HARUFU kwa kutumia pua; LADHA kwa kutumiamdomo/ulimi, KUGUSWA (touch) kwa kutumia ngozi, KUONA kwa kutumia macho, KUSIKIA kwa kutumia masikio. Lakini kwa mashushushu wanapaswa kuwa na hisia ya ziada ya kutambua kitu zaidi ya kutumia hisia hizo 5 kuu. Si kazi rahisi hata kidogo.
PART 2
Nianze sehemu hii ya pili ya mfululizo huu kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa wote waliowasiliana nami kuhusiana na mada hii. Kutokana na mawasiliano hayo, nimetambua kuwa mada hii ina umuhimu wa aina yake. Nami ninaahidi kuwaletea kitu kilicho bora kabisa, kwa maana ya 'darasa' kamili lakini pasipo kukiuka wala kukizana na sheria au taratibu zinazolinda fani hii nyeti.
Katika sehemu hii ya pili, tutaangalia jinsi afisa usalama wa taifa anavyopatikana, au kwa kimombo ni recruitment process. Ni muhimu kueleza kwamba taratibu za kujiunga na taasisi za usalama wa taifa duniani kote hupaswa kufanywa kwa umakini mkubwa hasa kwa vile majukumu na wajibu wa shushushu kwa taifa yana umuhimu mkubwa sana.
Kwa nchi 'za wenzetu' kama Marekani na Uingereza, zoezi la uajiri hufanyika kwa uwazi kidogo, kwa maana kwamba matangazo ya nafasi za kazi huwekwa hadharani. Mifano hai ni matangazo ya ajira za ushushushu katika tovuti ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Shirika la Ujasusi la Uingereza (MI6)
Kwa huko nyumbani Tanzania, zoezi la uajiri wa mashushushu hufanyika kwa usiri mkubwa (angalau taratibu zinapaswa kuwa hivyo). Na hata kwa mashirika ya kishushushu ya nchi nyingine, ajira za wazi kama nilivyoonyesha hapo juu hazimaanishi kuwa waajiriwa wote wa mashirika hayo hupatikana kwa uwazi.
Kimsingi, na pengine tukitumia mfano 'mwafaka' wa Idara yetu ya Usalama wa Taifa huko nyumbani, kinachoangaliwa kwa mtu anayetakiwa kuajiriwa ni 'vitu vya ziada' pengine tofauti na watu wengine. Katika mazingira stahili (ideal situation) shushushu mtarajiwa anatarajiwa kuwa na uwezo mkubwa wa akili, yaani kama nilivyoeleza katika makala iliyopita kwamba kazi yenyewe ni ya matumizi makubwa ya akili, kwahiyo mtarajiwa anapaswa kuwa intelligent kweli kweli.
Tukiendelea na mazingira hayo stahili, taasisi ya ushushushu huanza kitambo 'kumwinda' wanayetaka kumwajiri. Sehemu mwafaka zaidi za kusaka mashushushu watarajiwa ni katika taasisi za elimu. Sababu kuu za msingi za kutumia taasisi za elimu kama 'soko' la 'kuchagua mashushushu watarajiwa' ni, kwanza, umri wa wanafunzi wengi huwa mwafaka kuonyesha tabia zao halisi, na pili, taasisi ya elimu hutoa ushahidi mzuri wa kiwango cha akili cha shushushu mtarajiwa.
Sehemu nyingine iliyokuwa mwafaka kuwasaka mashushushu watarajiwa ilikuwa kwenye kambi za jeshi la kujenga taifa. Wakati taasisi za elimu zinatoa fursa nzuri kutambua uwezo wa akili wa shushushu mtarajiwa, kambi za JKT zilikuwa zikitoa fursa nzuri ya kuangalia uwezo wa kimwili, hususan uvumilivu (indurance). Kwa waliobahatika kupitia JKT wanafahamu bayana kuwa mafunzo ya awali (takriban miezi 6 ya mwanzo) yalikuwa yanaufikisha mwili katika kiwango cha juu kabisa cha uvumilivu. Ni katika mazingira kama hayo ndipo taasisi za kishushushu zinaweza kupata fursa ya kuona 'uwezo wa ziara' au 'usio wa kawaida' wa shushushu mtarajiwa.
Kadhalika, zamani kulikuwa na shule mbili-katika-moja iliyokuwa na mchepuo wa kijeshi. Shulke hiyo ni Tabora School, ambayo kimsingi ni Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana (Tabora Boys) na Tabora Wasichana (Tabora Girls). Shule hizi ambazo kimfumo zilikusanya wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao kutoka takriban kila wilaya ya Tanzania zilitoa fursa nzuri kwa Idara ya Usalama wa Taifa kupata maafisa wake watarajiwa. Uzuri wa shule hizo ni kwamba zilitoa fursa mbili kwa mpigo: fursa kwa mashushushu kupima uwezo wa kiakili wa mtarajiwa na pia kuona uwezo wake kimwili kupitia mazoezi na mafunzi ya kijeshi katika shule hizo. Vilevile, shule hizo ambazo pia zilikuwa na maafisa wa jeshi kama walimu, na wanafunzi wanaovaa sara zinazofanana na za kijeshi , zilitawaliwa na nidhamu ya hali ya juu, sambamba na kuhimiza uzalendo.
Lakini kwa vile ajira katika taasisi za kishushushu inazingatia zaidi mahitaji ya kimazingira, nyakati nyingine walengwa huwa watu waliopo makazini, kwa mfano wahadhiri, maafisa wa vyombo vingine vya dola - kwa mfano jeshi au polisi- na maeneo mengineyo. Ila ajira za namna hii ni za nadra kwa sababu mara nyingi watu wa aina hiyo 'huajiriwa' kama 'watoa habari' au sources kama wanavyofahamika kiintelijensia. Kinachoweza kuiskumua taasisi ya kishushushu kulazimika kumwajiri mtu ambaye tayari ana ajira nyingine au yupo katika fani tofauti ni unyeti wa nafasi yake na umuhimuwa wake wa muda mrefu.
Njia hii ni kama ya dharura au ya katika mazingira maalumu kwani kuna ugumu wa kumshawishi mhusika akubali kuajiriwa, na pengine mtu huyo anaweza kuwa na mtandao mkubwa wa kijamii - kwa maana ya familia au marafiki - na hilo linafanya sharti kuu la ajira kwenye taasisi yoyote ya usalama wa taifa, yaani USIRI, kuwa mashakani. Ni rahisi kumkanya mwanafunzi wa sekondari, kwa mfano, kwamba asimwambie mtu yeyote kuhusu jukumu atakalokabidhiwa mbeleni, na akalihifadhi - pengine kwa vitisho- kuliko mtu mzima ambaye inaweza kumwia vigumu kumficha mkewe au marafiki wa karibu. Na kama tujuavyo, ajira katika sehemu hizo zina 'ujiko' wa namna flani, kwahiyo si ajabu mtu mzima akiambiwa 'kuna dili' sehemu akaanza kutangaza kabla hata hajapewa mafunzo.
Kimsingi hakuna muda maalumu wa kumfuatilia mtu anayetakiwa kujiunga na taasisi ya kishushushu. Panapo dharura, zoezi la ufuatiliaji laweza kudumu kwa muda mfupi, lakini pasipo haraka yaweza kuchukua miaka kadhaa.
Baada ya kuwatambua 'waajiriwa watarajiwa' - process inayofahamika kama spotting - hatua inayoweza kufuata ni kuwa kuwaendeleza watarajiwa hao (yaani kuwaandaa kwa ajili ya utumishi kwa taasisi husika). Neno mwafaka ni development. Katika hatua hii, mashushushu HALISI wanakutana na mashushushu watarajiwa. Hatua hii inaweza kuchukua muda mfupi kutegemea mabo kahdaa au yaweza kuchukua muda mrefu pia. Hadi hapo, taasisi husika huwa haijafikia uamuzi wa kumwajiri mtarajiwa au la, bali inafanya marejeo ya ufuatiliaji wa awali na maendeleo ya mhusika katika kipindi hicho.
Sambamba na hatua hiyo, ni uamuzi kwa taasisi ya ushushushu kuanza kufanya ufuatiliaji wa kina kuhusu mtarajiwa. Ufuatiliaji huo hujulikana kama VETTING. Hata hivyo, uamuzi wa kufanya vetting hutarajia 'potential' ya mtarajiwa, hasa ikizngatiwa kuwa vetting ni process ndefu na inayoweza kuwa na gharama kubwa. Kwa kifupi, process hiyo inalenga kumfahamu mtarajia 'nje ndani' yaani kila kitu kumhusu yeye. Na hapo ndipo utabaini urahisi wa kutafuta mashushushu wapya wakiwa wadogo mashuleni- kwa vile hufanya vetting kutokuwa ndefu sana kutokana na kutokuwa na mtandao mkubwa wa mahusiano kijamii au kimaisha, ilhali kwa mtu mzima kazini itamaanisha kuwafuatilia watu wengi na pengine kutembelea sehemu nyingi pia. Na pindi vetting isipofanywa kwa umakini, dhamira nzima ya kufanya suala hilo kwa usiri linaweza kuathiriwa. Athari hizo si kwa taasisi ya kishushushu pekee bali pia yaweza kuyaweka maisha ya mtarajiwa hatarini.
Matokeo ya jumla ya vetting ndiyo yatakayoamua hatma ya ajira ya shushushu mtarajiwa. Nimesema 'matokeo ya jumla' kwa sababu hata baada ya kuajiriwa, shushushu huendelea kufanyiwa ufuatiliaji na mwajiri wake katika muda wake wote wa utumishi wake, na pengine hadi atakapoaga dunia. Kadhalika, vetting hujitkeza pia pindi shushushu anapotaka kuoa au kuolewa, ambapo mwenza wake hufanyiwa uchunguzi ili kuthibitika kuwa hatokuwa na madhara kwa utendaji wa kazi wa shushushu husika.
PART 3
Nianze makala hii kwa kuomba samahani kutokana na kuchelewesha mfululizo huu wa makala kuhusu taaluma ya ushushushu. Baadhi ya wasomaji wamehoji ukimya huo, huku wengine wakidhani kwamba 'wahusika' wamenizuwia. Ninapenda kurejea nilichokiandika katika sehemu ya kwanza ya makala hii kwamba mfululizo huu unazingatia sheria na maadili na 'wahusika' hawana sababu ya kuuzuwia.
Kwa kukumbushana tu, sehemu ya kwanza iliitambulisha taaluma ya ushushushu kwa ujumla, wakati sehemu ya pili ilielezea jinsi mashushushu wanavyopatikana (recruitment). Katika sehemu hii ya tatu tutaangalia mafunzo ya mashushushu wanafunzi.
Ninakumbuka siku moja niliwahi kuulizwa swali na rafiki yangu flani huko Twitter iwapo walinzi wa viongozi (bodyguards) nao ni mashushushu kwa maana ya kupitia mafunzi kama 'mashushushu wa kawaida.' Jibu langu kwake litatoa mwelekeo wa makala hii, kwamba, kwanza japo taaluma ya ushushushu ina maeneo flani yanayofanana mahala popote pale duniani, vitu kama mazingira, mahitaji ya nchi/taasisi ya kishushushu, na pengine uwezo wa kiuchumi hupelekea tofauti kati ya taasisi moja na nyingine. Nitoe mfano. Kwa nchi kama Marekani, taasisi ya kishushushu inayohusika na ulinzi wa viongozi (US Secret Service) 'inajitegemea' kwa maana ya ajira,mafunzo na utendaji kazi. Wanaojiunga na taasisi hiyo ni lazima wapitie kozi ya awali ya upelelezi wa jinai (Basic Criminal Investigator Training) inayodumu kwa wiki 10, na inayofanyika katika chuo cha Federal Law Enforcement Training Centre kilichopo Glynco, Georgia, na kisha kufanya kozi nyingine ya wiki 17 inayojulikana kama Speicla Agent Basic Training, inayofanyika katika chuo cha James J. Rowley Training Centre, nje kidogo ya jiji la Washington DC.
Kwa minajili ya kuepuka mkanganyiko, nitatumia mfumo unaotumiwa na Idara yetu ya Usalama wa Taifa (TISS) katika maelezo kuhusu mafunzo ya mashushushu. Tofauti na Marekani, Idara yetu ya Usalama ni taasisi moja yenye vitengo mbalimbali. Na katika jibu nililompatia rafiki yangu ailiyeniuliza huko Twitter, maafisa usalama wanaolinda viongozi wetu huajiriwa kama afisa usalama mwingine yeyote yule. Katika mazingira ya kawaida, baada ya Idara ya Usalama wa Taifa kumaliza mchakato wa kuwapata mashushushu watarajiwa (process niliyoieleza kwa undani katika makala iliyopita), hatua inayofuata ni mafunzo.
Kwa huko nyumbani, kila shushushu mpya hupatiwa mafunzo kupitia kozi ya awali ya uafisa (Junior Basic Course) katika chuo chao kilichopo pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam. Urefu wa kozi hutegemea vigezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya Idara yenyewe.
Muundo wa mafunzo:
Kimsingi, na katika mazingira ya kawaida, kozi hiyo ya awali hugawanywa katika sehemu kuu tatu: mafunzo ya kijeshi na ukakamavu, mafunzo ya mapambano pasipo silaha (unarmed combat) na mafunzo ya ushushushu 'halisi.'
Mafunzo ya kijeshi na ukakamavu hujumuisha 'kwata' za kijeshi (kama zile wanazofunzwa 'makuruta' katika Jeshi la Kujenga Taifa). Kabla ya kuanza kozi hii, mashushushu watarajiwa hufanyiwa uchunguzi wa kiafya kubaini iwapo wataweza kumudu shuruba zinazoambatana na kozi hiyo. Na kwa hakika ni hatua ngumu mno, ambapo kwa takriban kila 'intake' kuna 'wanafunzi' wanaoamua kuomba ruhusa ya kuondoka baada ya kushindwa kustahilimi ugumu wa mafunzo hayo.
Haya ni mafunzo ya kijeshi 'halisi' kwa maana ya drills za kijeshi, mafunzo ya msingi ya kivita ikiwa ni pamoja na usomaji ramani katika uwanja wa mapambano, ulengaji shabaha, uelewa kuhusu silaha mbalimbali, nk. Sambamba na mafunzo hayo ni mazoezi makali ya viungo na ukakamavu. Kadhalika, mafunzo hao huambatana na kujenga nidhamu ya kijeshi pamoja na uvumilivu (ni jambo la kwaida kwa 'wanafunzi kupitisha usiku kadhaa bila kulala). Mafunzo haya huendeshwa na wakufunzi wa kijeshi ambao pia ni waajiriwa wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Hatua inayofuata ni kozi ya mapambano bila silaha (unarmed combat). Katika kozi hii, mashushushu watarajiwa hufundishwa jinsi ya kupambana na adui kwa kutumia mwili pekee, yaani bila kuwa na silaha. Walimu wa kozi hii huitwa Sensei na kozi hujanyika katika ukumbi ujulikanao kama dojo. Kadhalika, 'wanafunzi' huvaa ' mavazi maalum' yajulikanayo kama Kimono.
Pasipo kuingia ndani zaidi, kozi hii hufuata mfululizo wa hatua zinazojulikana kama 'kata.' Kwa lugha nyepesi, kata ni movements za mtu mmoja mmoja au zaidi, na kila moja ni mfumo wa mapambano. Kila kata ina jina, na majina hayo yana asili ya Mashariki ya Mbali, ambapo fani ya mapambano bila silaha ni sehemu muhimu ya utamaduni kwa nchi kama China,Japan, Korea, nk. Ili kujifunza kata inayofuata ni lazima kuimudu kata ya awali. Ni kama vile hatua za makuzi ya mtoto, hawezi kuanza kukimbia kabla ya kutamaa.
Kwa minajili ya kurahisisha maelezo, kozi hii hujumuisha karate, judo,ngumi,nk. Kadhalika, japo mafunzo yanaitwa mapambano bila ya silaha, ukweli ni kwamba kuna baadhi ya kata huhusisha matumizi ya/ kujilinda dhidi ya silaha ndogo japo hatari kama vile visu, jambia la mapambano, minyororo, nk. Katika kozi hii, 'wanafunzi' hufunzwa pia kuhusu 'sehemu za udhaifu katika mwili wa binadamu' (weak points) kwa minajili ya kutambua eneo gani la mwili wa adui likidhibitiwa anakuwa 'hana ujanja.'
Hatua ya tatu ni mafunzo 'halisi' ya ushushushu. Kwa ujumla, mafunzo haya humfundisha shushushu mtarajiwa mbinu za kukusanya taarifa za kiusalama kwa siri, kuzichambua na 'kuzifanyia kazi.' Kwa ujumla pia, kozi hii hugawanywa katika makundi mawili: ushushushu ndani ya nchi na ujasusi ushushushu nje ya nchi. Kadhalika, masushushu wanafunzi hufunzwa kitu kinachoitwa 'shughuli za adui' yaani ujasusi (espionage), uzandiki (subversion), hujuma (sabotage) na ugaidi (terrorism). Vilevile, hufunzwa mbinu za kunasa mawasiliano (bugging), ufuatiliaji wa siri (surveillance), jinsi ya kupata watoa habari (recruitment of sources) na jinsi ya kuwamudu, ikiwa na pamoja na jinsi ya 'kuwamwaga' (kuachana nao) pale wanapopoteza umuhimu.
Pengine la kuchekesha katika hatua hii ya mafunzo ya ushushushu ni hisia kwamba 'mashushushu hufundishwa kutongoza.' Kuna aina flani ya ukweli katika hilo japo kinachofundishwa sio jinsi ya kutongoza mwanamke bali kutongoza kwa minajili ya kupata taarifa. Na pengine neno 'kutongoza' sio stahili kwani lina connotation na mambo ya ngono.
Japo mbinu za kukusanya taarifa za kiusalama (methods of elicitation) ni maalum kwa matumizi ya mashushushu, kimsingi zinatumika katika fani nyingine, kwa mfano watafiti wanapofanya mahojiano kwa ajili ya tafiti zao.Tofauti ya msingi ipo kwenye usiri unaoambatana na mbinu husika, kwa mfano mtu kuhojiwa pasi kujua anahojiwa na shushushu. Mfano mmoja wa mbinu hizo ni kinachotwa 'incorrect supposition.' Mbinu hii inatumia udhaifu wa kawaida wa binadamu kutotaka kuelezwa isivyostahili. Kwa mfano, katika kutaka kufahamu kama mtumishi wa kawaida tu ana 'fedha zaidi ya uwezo wake.' shushushu anaweza kumwambia mtu huyu "ah inadaiwa wewe ni masikini tu ambaye hata kodi ya nyumba ya kupanga inakusumbua." Katika mazingira mwafaka, mhusika atakurupuka na kujigamba, "ah wapi bwana. Utawaweza waswahili kwa uzushi? Mie nina nyumba kadhaa hapa mjini, na lile duka la spea pale Kariakoo ni langu..." Kwahiyo wakati mwingine ukiskia mtu anang'ang'ania kusema kitu kisicho sahihi dhidi yako, usikimbilie kudhania anakudhalilisha au hajui ukweli.Yawezekana 'anakulengesha' umpatie ukweli anaohitaji.
Mbinu nyingine ni ya 'nipe nikupe.' Nakupa unachodhani ni taarifa za siri (naam, pengine ni za siri kweli lakini hazina madhara) ili nawe unipe taarifa ninazohitaji. Ni kile wanaita 'Quid Pro Quo.'
Jambo jingine ambalo mashushushu wanafunzi hufundishwa muda wote ni kitu kinachofahamika kama constant vigilance of an officer, yaani afisa usalama wa taifa anapaswa kuwa macho muda wote, huku akitambua kuwa uhai wa taifa lake upo mikononi mwake muda wote. Pengine tafsiri ya kanuni hiyo ni 'kujitambua muda wote.' Kutambua dhamana aliyonayo afisa usalama kwa taifa. Kadhalika, mafunzo huhusisha pia kujenga na kuimarisha matumizi ya 'hisia ya sita.' Kama nilvyoeleza katika makala ya kwanza, binadamu tuna hisia tano: kuona kwa kutumia macho, kusikia kwa kutumia masikio, kunusa kwa kutumia pua, ladha kwa kutumia ulimu na kuguswa (touch) kwa kutumia ngozi. Hisia ya sita ni kitu cha zaida ya hivyo vitano. Ni vigumu kueleza katika mazingira ya kawaida ila labda kwakifupi ni ule uwezo wa kwenda mbali zaidi ya uwezo wa kawaida wa hisia: kuamini au kutoamini pale inapopaswa kuamini au kutoamini, kutambua hatari hata bila ya kupewa tahadhari, nk.
Awali nimetaja kuhusu vitendo vya adui, yaani ujasusi, uzandiki, hujuma na ugaidi. Kimsingi japo hivi ni vitendo vya adui na njia ya kupambana nayo ni kinachojulikana kama counterintelligence au CI kwa kifupi, mashushushu wanafunzi hufunzwa pia mbinu 'za kiadui.' Ni hivi, kuna nyakati serikali au taasisi ya usalama hulazimika kupelekea amshushushu wake nje ya nchi, na kimsingi hawa ndio wanaoitwa spies, na kitendo chenyewe ndio espionage (ujasusi), lengo si 'kutengeneza maadui' bali kuwapatia mashushushu uwezo wa kukusanya taarifa za kiusalama nje ya nchi. Miongoni mwa kanuni anazofundishwa shushushu mwanafunzi ni pamoja na uwezekano wa kukanwa na nchi yake pindi akikamatwa kwenye operesheni za nje ya nchi. Vilevile, mashushushu hufunzwa kuhusu kitu kinachofahamika kama 'kifuniko' (cover ) yaani utambulisho bandia. Kwa mfano, balozi takriban zote duniani huwa na majasusi wanaojipachika vyeo kama 'mwambata wa siasa' au mwabata wa ulinzi.' Ieleweke kuwa japo ushushushu ni fani inayokubalika, serikali rafiki ikitambua shughuli za maafisa usalama wa nchi nyingine rafiki, yaweza kupelekea matatizo makubwa. Na mara nyingi ukisikia serikali imewafukuza maafisa ubalozi flani basi mara nyingi watu hao ni mashushushu 'waliojificha' kama maafisa ubalozi.
Vilevile, katika muda wote wa mafunzo, mashushushu watarajiwa huhamasishwa kuhusu uzalendo, thamani ya nchi yao, umuhimu wa kuilinda muda wote, umuhimu wa taaluma hiyo katika ustawi na mustakabali wa taifa lao,nk. Na siku ya kuhitimua mafunzo, kila shushushu huapa kwa kushika alama muhimu za taifa- katiba/bendera ya taifa, na kuweka kiapo cha kuitumikia nchi yake kwa uwezo wake wote, sambamba na viapo vingine vya kikazi (kwa mfano kamwe kutotoa siri za nchi na za Idara). Japo kuna hisia 'mtaani' kwamba watu walioacha au kuachishwa ushushushu huogopa kutoa siri kwa kuhofia kuadhibiwa, ukweli ni kwamba kiapo wanachokula wakati wa kuhitimu mafunzo ni 'kizito' mno kiasi kwamba katika mazingira ya kawaida, mhusika atajiskia nafsi inamsuta kusaliti kiapo hicho.
Licha ya mafunzo ya darasani, kuna mafunzo ya nje ya darasa ambapo mashushushu watarajiwa 'humwagwa mtaani' kufanya mafunzo ya vitendo.
Kubwa zaidi wakati mafunzo yanaendelea ni usiri wa hali ya juu. Katika mazingira ya kawaida, kila shushushu mwanafunzi huwa amefika ukweli kuwa anaenda/ yupo mafunzoni. Na kuficha huko si kwa marafiki tu bali hata wazazi na ndugu wa karibu. Na hapa ni muhimu kueleza kwamba moja ya vitu anavyokumbushwa afisa usalama wa taifa tangu hatua za mwanzo za kujiunga na taaluma hiyo hadi katika maisha yake ya kila siku ni KUWA MAKINI NA IMANI, au kwa lugha nyingine USIMWAMINI MTU YEYOTE. Wanasema TRUST WILL GET YOU KILLED, yaani IMANI (kwa mtu au kitu) ITAKUUWA. Kwahiyo si jambo la ajabu kwa shushushu kutomwamini hata mzazi, ndugu au mwenza wake.
Naweza pata Kitabu Juu Usalama wa Taifa kama hapo juu unavyoelezea kiundani zaidi, Pia Tanzania hapa wapi private unaweza kufundishwa na ukawa mwanausalama???
ReplyDeleteNaweza kupata kitabu hicho
ReplyDeleteThanks
ReplyDeleteNmeipenda hii makala na imenipa hamu ya kuchimba zaidi hizi mambo zinavyo operate hapa kwetu na nchi zingine zilizo endelea
ReplyDelete