Tuesday, 2 August 2016
Home »
Siasa
» Soma historia hii ya Burundi utajifunza kitu ndani yake dhidi ya mapinduzi ya Nkurunziza
Soma historia hii ya Burundi utajifunza kitu ndani yake dhidi ya mapinduzi ya Nkurunziza
Burundi nchi ndogo iliopo katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ilikaliwa na wakoloni wa Kibeligiji na kujikuta ikipita kwenye jangwa la harubu na misukosuko mingi ikiwamo ya umwagaji wa damu.
Hali hiyo imetokana na kuzuka vita ya kikabila viliyoacha makovu, machungu na kumbukumbu mbaya katika uga na mwelekeo wa maendeleo ya siasa na demokrasia yake hata kutishia na kuathiri nchi jirani ikiwamo Tanzania.
Chimbuko la ghasia na mapigano inaelezwa kuwa ni Jeshi la Burundi kuasi na kusababisha mauaji ya kinyama kwa wananchi wasio na hatia.
Ufalme, mapinduzi ya kijeshi
Julai mosi, 1962, Burundi ilipata uhuru. Lakini katika miaka hiyo ya 1960, ilitawaliwa na mapigano yaliyohusisha Wahutu na Watutsi. Mwaka 1965 kulitokea jaribio la mapinduzi lililofanywa na Wahutu na kusababisha Watutsi walipe kisasi kwa kuwaua Wahutu wengi.
Julai 1966, Mfalme Mwambutsa wa IV alipinduliwa na mwanawe aliyefanywa kuwa Ntare wa V. Naye alipinduliwa katika mapinduzi ya kijeshi ya Novemba 1966.
Michel Micombero, ambaye alikuwa amechaguliwa Waziri Mkuu mwaka 1966, akawa rais na Katiba Mpya ikaanzishwa mwaka 1970.
Micombero naye alipinduliwa na Kanali Jean-Baptiste Bagaza, pia Mtutsi, ambaye aliimarisha utawala wa Kitutsi madarakani.
Ni nchi hiyo iliandamwa na matukio ya kupinduana madarakani, kuzingwa na kadhia ya ukabila na mapigano ya silaha tokea ilipopata uhuru wake, baada ya kuanguka kwa ukoloni.
Kiasili Warundi ni wakulima wa kahawa aina ya arabika na robusta, wakati kipato cha mwananchi kinakadiriwa kuwa chini ya Dola moja ya Marekani kwa siku.
Makabila makubwa nchini Burundi ni Wahutu wanaochukua asilimia 90 ya wananchi wote, wakati asilimia tisa ni Watutsi na waliobaki ni kabila dogo la Watwa.
Takwimu za mwaka 2005 zinaonyesha kuwa nchi hiyo ilikuwa na wananchi wapatao milioni saba, idadi ambayo bila shaka imeongezeka.
Historia inaonyesha kuwa Watutsi ndiyo waliokuwa wakazi asilia wa Burundi, lakini idadi yao ilizidiwa na Wahutu. Katika karne ya 15, Watusi waliingia eneo hilo na kuwazidi Wahutu nguvu ya kiutawala. Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, majeshi ya Ubeligiji yaliitwaa Burundi mwaka 1916 na mwaka 1919 nchi hiyo ikawa sehemu ya himaya ya Ubeligiji.
Kushamiri vita na marais watano
Kushamiri vita ya kikabila kulishuhudia raia wengi wa makabila makuu ya nchi hiyo; Wahutu na Watutsi wakiuawa kinyama.
Kwa nyakati zote za vita na machafuko, nchi hiyo iliongozwa na Michael Micombero; Jean Babtist Bagaza, aliyefuatiwa na Pierre Buyoya kabla ya Melchior Ndadaye ambaye awali alianzisha kundi la msituni akilenga kusaidia na kulinda haki za Wahutu.
Siku chache baada ya ushindi wa Ndadaye, kupitia chama chake cha Frodebu, Julai 10, 1993 aliapishwa na kuwa rais wa kwanza wa kuchaguliwa huku akimteua Alphonce Kadege kutoka chama cha upinzani cha Uprona, kuwa makamu wake.
Ndadaye aliyezaliwa Machi 28, 1953 katika Mkoa wa Muramvya, ni msomi aliyepata elimu ya msingi kwenye mji wa Mbogora, mkoani Gitega mwaka 1960 hadi 1966. Pia alipata masomo ya juu na baadaye akawa mwalimu na mtumishi wa benki.
Uchaguzi wa 1993, ndiyo uliomwingiza madarakani Ndandaye, baada ya kumbwaga Buyoya aliyekuwa ofisa mkubwa wa Jeshi la Burundi.
Katika utawala wake Ndadaye aliwashirikisha wapinzani katika Serikali yake hali iliyoleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Burundi, huku kwa muda wa miezi mitatu yakishuhudiwa mabadiliko makubwa ya miundombinu na huduma za kijamii kutokana na kufuta sera za kikabila.
Wimbi la mauaji
Lakini kama ilivyo kwa msemo wa Waswahili; Kizuri hakidumu, ghafla ndoto ya Warundi kuingia katika utawala bora, ilizimika.
Ulikuwa ni usiku wa mshtuko kwao, Afrika na dunia nzima pale Redio ya Taifa ilipotangaza asubuhi kuwa Rais Ndadaye ameuawa na askari wa Kitutsi, walioamua kuasi katika makazi yake jijini Bujumbura. Mauaji yake yaliibua wimbi la mauaji ya kinyama dhidi ya Wahutu na wanajeshi wa Serikali kutajwa kuhusika, hadi kuthubutu kuipindua Serikali ya kiraia katika mapinduzi yaliyofanikishwa na Meja Buyoya kwa mara nyingine.
Ndadaye aliuawa usiku wa manane nyumbani kwake, miezi mitatu tangu kuchaguliwa kwake, baada ya Chama cha Frodebu, kujipatia ushindi mkubwa kilipokibwaga Chama cha Watutsi, Uprona, kilichokuwa madarakani chini ya uongozi wa Charles Mukasi.
Kuingia madarakani kwa Buyoya, kulizusha vikundi zaidi vya uasi hali iliyoisukuma jumuia ya kimataifa kuingilia kati na baadaye hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akawa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi.
Hata hivyo, mauji ya mwaka 1994 hayakuwa ya kwanza kwa Burundi iliyojiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki miaka miwili iliyopita.
Kwake misukosuko ya mauaji kikabila ilianza mwaka 1972 pale Wahutu waliokuwa wengi jeshini, walipopindua Serikali ya Watutsi waliokuwa wameshika hatamu ya uongozi chini ya Rais Michael Michombero.
Kwa sasa mapigano ya kikabila yamepungua, lakini zipo taarifa za chini chini kuwa hali ya mambo si shwari na tayari imezusha hofu kwa wananchi waliokuwa wamesahau machafuko.
Katiba na Bunge
Burundi inatawaliwa kwa kutumia Katiba ya mwaka 2005, inayoelekeza kuwa kutakuwa na Uchaguzi wa Rais, kila baada ya miaka mitano.
Bunge la Burundi lenye viti 100, lina asilimia 60 ya wawakilishi Wahutu na asilimia 40 ni Watutsi. Asilimia 30 ya wawakilishi bungeni ni wanawake.
Pamoja na hali ya kisiasa kuwa ngumu na mbaya kwa miaka kadhaa, hatimaye mwaka 2005 Burundi ikafanya uchaguzi wake kwa njia ya kidemokorasia ulikokiweka madarakani Chama cha CNDD FDD kilichokuwa msituni kwa miaka 10 na kumteua Pierre Nkurunziza kuwa mgombea wake wa urais.
Awali, Nkurunziza alihesabika kama mwanachama mwalikwa aliyekaribishwa kwenye chama hicho kilichoanzishwa na waasi wa CNDD FDD, chini ya kiongozi wake mkuu, Hussein Rajab ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Nkurunzinza.
Chini ya utawala wa Nkurunziza, Rajab alikamatwa na kufunguliwa kesi na kufungwa gerezani miaka 15, hadi pale alipotoroka miezi kadhaa iliopita akisindikizwa na vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi hiyo hadi mafichoni aliko hadi sasa.
Hatua ya mfungwa wa kisiasa kutoroka gerezani ni alama mbaya kwa Rais Nkurunziza, kwani hata vyombo vya dola havikuwa pamoja naye ndiyo maana Rajab alifanikiwa kutoroka akiwa katika ulinzi mkali.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi za Maziwa Makuu zimechelewa kuzima cheche za kuvuruga amani ya Burundi zilizoanza kuonekana mapema kwa kukamatwa wanasiasa tishio kwa Nkuruziza, bila ya yenyewe kukemea au kuchukua hatua stahiki.
Kisiasa tukio hilo la kutoroka gerezani kwa Rajab lilitosha kwa Rais Nkurunziza kusoma alama za nyakati kwani mwanasiasa huyo amekuwa na mvuto na ushawishi mkubwa katika siasa za Burundi na ndani ya CNDD.
Pengine Nkurunziza alipaswa kubaini kuwa kwa tukio hilo, lolote lingeweza kutokea na pengine kutumia busara, kubatilisha mpango wake kuwania tena muhula wa tatu wa urais kama alivyokusudia.
Hali hiyo ilizua maandamano kwa wanasaisa na wananchi wakipinga nia yake kuwania tena urais hata kuwasukuma wakuu wa nchi za EAC kuitisha mkutano jijini Dar es Salaam kujadili mustakabali wa nchi hiyo.
Mei 13, Meja Jenerali Godefroid Nyambare wa Jeshi la Burundi alitangaza kupitia kituo kimoja cha redio binafsi kuwa utawala wa Nkurunzinza umekoma na kuangushwa.
Tukio hilo lilitokea wakati Nkurunzinza akiwa jijini Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo.
Hata hivyo, jaribio hilo ambalo lilishindwa lililaaniwa vikali na viongozi wa EAC ambao pamoja na mambo mengine walishauri kwamba uchaguzi usogezwe mbele nchini Burundi wakati vikundi hasimu vikitafuta suluhu ya matatizo yaliyojitokeza.
0 comments:
Post a Comment