Recent

JIFUNZE MAMBO MBALIMBALI YATAKAYOKUPA MAARIFA NA UJUZI MAISHANI

Thursday, 1 September 2016

Ngassa avunja mkataba na Free State baada ya kukerwa na kocha mfaransa


KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa si mchezaji tena wa Free State Stars ya Afrika Kusini.

Hiyo inafuatia mchezaji huyo wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba, Yanga SC, Azam FC na Simba za Dar es Salaam kuvunja mkataba na klabu hiyo leo mchana.

Meneja Mkuu wa Free State Stars, Rants Makoena alikuwa na kikao kirefu na Ngassa leo makao makuu ya klabu, Mtaa wa President Boshoff Bethlehem, Afrika Kusini wakijadili masuala mbalimbali kabla ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba.

“Ngassa alikuwa ana hoja zake kama mchezaji akitaka kuvunja mkataba, baada ya majadiliano marefu, kiungwana tukakubaliana naye. Tunamtakia safari njema, hatuna kinyongo naye,”alisema Mokoeana

Habari za ndani zinasema mwezi wote wa Agosti Ngassa amekuwa akishinikiza kuondoka Free State na baada ya uongozi kuhisi hauwezi kumzuia tena ukamleta Hamisi Kiiza, mchezaji mwingine wa zamani wa zamani wa Simba na Yanga ambaye tayari amejiunga na timu hiyo.

Kwa upande wake, Ngassa alisema kwamba sababu kubwa za kuondoka Free State ni timu ambayo haina malengo ya kushinda taji.

“Ninapenda kushinda mataji, nimezoea kushinda mataji tangu nipo mdogo, na nina rekodi ya kushinda mataji tangu klabu yangu ya kwanza ya Ligi Kuu (Kagera Sugar). Ninaondoka Free State kwenda kujiunga na klabu ambayo itanirejesha kwenye enzi za kushinda mataji,”alisema Ngassa.

Alipoulizwa ni timu gani anakwenda baada ya kuondoka Free State Stars, Ngassa alisema; “Utaijua baada ya muda si mrefu,”. 

Ngassa alijiunga na Free State Stars Mei mwaka jana akisajiliwa na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri kwa mkataba wa miaka minne.

Hata hivyo, kocha aliyemsajili baba huyo wa Farida (9) na Faria (7) alifukuzwa baada ya miezi miwili tu.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa kuwa Free State, Ngassa amefanya kazi na makocha wanne akiwemo huyu wa sasa, Mfaransa Denis Lavagne aliyeanza kazi Juni mwaka huu.
Wengine ni Mjerumani Ernst Middendorp aliyefanya kazi kati ya Septemba na Desemba 2015, Mtaliano Giovanni Solinas aliyefanya kazi kati ya Desemba na Mei 2016.



Na Lavagne ndiye aliyechangia Ngassa kuomba kuondoka Free State baada ya kuonyesha kuidharau Tanzania haiwezi kuwa na mchezaji bora.

Lavagne alimuanzishia benchi Ngassa katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya ABSA ya Afrika Kusini Agosti 23, kabla ya kumuingiza dakika ya 63 kwenda kuchukua nafasi ya Mbuyiselo Thethani wakati huo tayari FS imekwishapigwa 2-1, matokeo yaliyodumu hadi mwisho wa mchezo.

Na baada ya kuingia Ngassa akaenda kucheza kwa kiwango kizuri na kukaribia kufunga mara mbili hadi kocha huyo akampongeza baada ya mchezo, ingawa tayari mchezaji wa Tanzania alikwishatumbukiwa nyongo na Mfaransa huyo.

Ngassa akazidisha shinikizo la kutaka kuondoka baada ya mchezo huo hatimaye leo amefanikiwa kuachana salama na klabu hiyo, iliyokaribia kuuzwa Julai kutokana na ukata.

0 comments:

Post a Comment