Salaam Ndugu
zangu Watanzania!!
Baada ya
uhuru, Baba wa Taifa la Tanganyika na baadae Tanzania Mwl.J.K Nyerere alijaribu
kuonesha dira na dhamila yake ya kujenga nchi ya kijamaa ambapo katika mfumo wa
kijamaa unalenga watu wake kujitegemea yaani kuishi kutokana na kazi za mikono
yao badala ya kusubiri wafanyiwe kazi.Mfumo wa kijamaa ni mfumo ambao unapinga
unyonyaji baina ya mtu na mtu.
Kwasababu dhamila ya Mwl.Nyerere
ilikuwa ni kujenga nchi ya viwanda aliweza kutenga shule zetu zikawepo shule za
ufundi ambazo baadhi ya shule hizo ni Ifunda
Technical, Tanga Technical, Moshi Technical, Iyunga mbeya na nyinginezo shabaha ya kuweka shule za namna hii
ilikuwa ni kuwaandaa vijana kuweza kuwa na ujuzi ambao wangeenda kuutumia
katika viwanda , kuonesha kwamba Mwalimu alikuwa anamaanisha na kudhamilia kuwa
na nchi ya kujitegemea alianzisha viwanda kama
Mwatex,Sungura,Urafiki na vingine vingi maana yake vijana waliokuwa
wakimaliza mafunzo hayo walifanya kazi katika viwanda hivyo na alifanikiwa kwa
kiasi kikubwa mpaka anastaafu ameacha
takribani viwanda kumi na viwili vikubwa na vingine vidogovidogo.
Lakini pia palikuwapo na shule za vipaji
maalum mfano Ilboru Arusha, Mzumbe Morogoro, Kibaha Pwani, Kirakala
Morogoro, Msalato na nyingine
kadhaa shabaha ya kuwa na shule hizi ilikuwa ni kuandaa viongozi wa nchi kwa
maana ya watungasela na viongozi wa juu kwaajili ya Taifa na mwisho palikuwepo
na shule za kawaida ambazo ziliitwa shule za wazazi ambazo kwa kiasi kikubwa
zilijengwa na wananchi wenyewe na baadae kuzikabidhi kwa serikali nazo zikawa
za serikali.Mfano wa shule hizo ni Lusanga
Sekondari Turiani Morogoro, Morogoro sekondari, Oldadai sekondari Arusha na nyingine nyingi.
Sasa nini maana ya haya yote ,kwa
mujibu wa mwanafalsafa maarufu duniani
kutoka katika nchi ya Athens PLATO
aliyezaliwa mwaka 428 kabla ya kristo (B.C) na mbaye pia alikuja kuwa
mwanafunzi wa Socrates yeye aliamini sana juu ya Hisabati, Sayansi na Elimu ya
Anga kuwa nyenzo muhimu ya kuwafanya watu wajue kufikiri vizuri vema pamoja na
imani hiyo lakini akawatenga watu katika makundi matatu juu ya uwezo wao wa
fikra na uwezo wa akiliyaani Intelligent Quotient(IQ) makundi hayo ni wenye IQ
ya juu zaidi akawaita (
Gold au Gifted), wenye uwezo wa kati
akawaita (Silver) na kundi la mwisho
ambao wanauwezo wa kawaida akawaita (Dulla
) na falsafa hii ndiyo Mwl.Nyerere aliyoitumia katika kupanga mfumo wa
elimu yetu ya Tanzania na mimi katika makala hii nitajikita kuzungumzia hawa wa
kundi la mwisho na umuhimu wao katika sera ya viwanda.
Gold, aina hii ya watu huwa wana uelewa
wa hali ya juu zaidi na wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo bila ya kufundishwa,
tatizo lao moja huwa hawaamini kama watu wengine hawaelewi, kwahiyo kundi hili
hawafai kuwa waalimu wanafaa kufanya mambo makubwa zaidi maana wakiwa waalimu
si rahisi wanafunzi kuwaelewa si kwamba hawajui wanachokifundisha bali kutokana
na kuwa na uelewa mkubwa huwa wanaharaka ya kufikia jambo mapema zaidi.
Silver,
hili nikundi la watu wenye uwezo wa kati lakini wakijibidisha zaidi wanawezakufanana
na wale wakundi la kwanza hawa huwa wanauwezo binafsi ambao wakikazana kwa
juhudi zao binafsi wanakuwa na uwezo sawa na wale wakundi la kwanza.Hili ndilo kundi
walipo Waalimu, maana kundi hili la watu wanaamini kuwa huwa kuna watu
hawaelewi hivyo kuenda nao taratibu na pale ambapo wanagundua kuwa wale wanao wafundisha
hawawaelewi huwa wanajitahidi kuwaelekeza zaidi ili wawaelewe.
Dulla, hawa ni aina ya watu wasio wazuri
sana katika elimu ya nadharia kwamaana ya elimu ya darasani tu bali aina ya
kundi hili la watu ni hodari sana katika shughuri za mikono na hasa zenye
kutumia nguvu na niwepesi sana katika shughuli za ufundi, majeshini aina hii ya
watu ni wengi sana simaanishi wote kuna vitengo vya kitaalam ambavyo hufanywa
na watu wachache na kazi nyingine za nguvu hufanywa na wao na pia shughuli
nyingine za mikono.
Nimeona nitoe falsafa hizo ambazo
zilitumika kupanga mfumo wetu wa elimu, hivyo basi ili nchi iweze kuwa nchi ya
viwanda ifanye nini sasa.
Kwanza tubadili aina ya mfumo wetu wa
elimu, badala ya kuwa na elimu ya nadharia tu inapaswa kuwa elimu ya vitendo
nikimaanisha VOCATIONAL TRAINING yaani
elimu yetu ya msingi iwe ni elimu ya ujuzi.
Shabaha ya elimu ya msingi hapo awali
haikulenga kuwaanda vijana kwenda sekondari bali iliwaanda vijana kujitegemea
baada ya masomo yao.Kwahiyo tusilazimishe kila mtu kwenda sekondari maana
kutokana na falsafa hizo hapo juu ni ukweli kwamba watu wanatofautiana uwezo wa
kuelewa na vipaji tofautitofauti kwanini tuamini kuwa lazima kila mtu afike
sekondari?Huu ni ujinga na sasa je akifika sekondari na kumaliza bila kuwa na
ujuzi wowote elimu yake itakuwa imemfaa nini?
Nadhani serikali katika hili inawajibu wa
kufikiri upya juu ya elimu yetu tusifanye mambo ya kutaka kuwafurahisha
wananchi kuwaonesha kuwa watoto wao wanakwenda sekondari lakini mwisho wa siku
hatuna habari na wale wanaofeli mwisho wa mwaka katika elimu yao ya sekondari.Maana
wakishafeli serikali huwa haiwatambui tena, linabaki suala la mzazi mwenyewe ajue atamsaidiaje mtoto wake, lakini hawa
vijana ndiyo wanapaswa kuwa viongozi na watendaji wa serikali hapo baadae
kwahiyo serikali inawajibu wa kuweka misingi ya kuwafanya wawe watu wa
kujitegemea baada ya masomo yao.
Inasikitisha sana mtu anasoma shule ya
msingi miaka 7 anamaliza bila ujuzi, anakwenda sekondari miaka 4 anamaliza bila
ujuzi, anakwenda kidato cha sita miaka 2 anamaliza bila ujuzi wowote halafu
utegemee asome kwa miaka 3 au 4 chuo kikuu awe na ujuzi wa kutosha kufanya
kazi? Kwa mtaji huu wasomi wa hapa nchini wataendelea kuwa washika mikoba ya
wataalamu kutoka nje ambao ujuzi wa elimu zao unatokana na kuwekeza kwa muda
mrefu katika elimu ya ujuzi wa shughuli za mikono.
Mfano tazama
contractor zinazochukuliwa na wageni hapa kwetu ni nyingi zaidi kuliko za
wazawa, maana yake nikwamba wazawa wengi wana alama nzuri sana kwenye
makaratasi ya vyeti vyao, lakini katika uhalisia wa ujuzi hakuna kitu pamoja na
kwamba wanadai kuwa kutoanzisha makampuni ya kujiajiri inatokana na kukosa
mitaji inawezekana lakini wangekuwa wanaujuzi wa kutosha tayari mtaji wangekuwa
nao maana mtaji ungekuwa ni ujuzi wao.
Kama
Taifa tunapaswa kwanza kuwa na aina ya mfumo wa maisha tunaouhitaji, kwenye
katiba ya nchi, katiba ya CCM chama kinachoongoza serikali na katika matamko
mbalimbali kama Azimio la Arusha yana itaja nchi ya Tanzania kama nchi ya
ujamaa na kujitegemea lakini matendo na maisha tunayoishi si ya mfumo wa
kijamaa.Kuwa na aina ya mfumo wa maisha katika taifa lolote ndiyo dira
inayotumika kupanga aina ya mfumo wa elimu tuipendayo.
Mfano, nchini UHOLLANZI kwa kutambua kuwa nchi yao imezungukwa na maji kila kona
basi katika mtaala wao wa elimu wameingiza suala la kujenga mabwawa (Swimming
pool) kwajili ya watoto wao kujifunza namna ya kuogelea ili siku ikitokea nchi
yao imezama baharini au wakati barafu zikiyeyuka basi kila Raia awe na uwezo wa
kuogelea na kujiokoa, sasa Tazania hatueleweki katiba inatamka juu ya ujamaa
lakini matendo na maisha yanaonekana kuwa ya kibepari.
Mfano,
kuwa na shule za binafsi na zenye ubora zaidi kuliko za umma ni jambo la kibepari
maana watu sasa hatupati elimu inayofanana katika misingi ya ujamaa na
kujitegemea lakini haitoshi tu bali mfumo huu wa sasa unatengeneza watu
waliokwenda shule kujiona mabwana na wengine kuonekana watumwa na wenye mawazo ya kuajiriwa zaidi badala ya
kujiajiri wenyewe.
Tahadhari yangu tu kwa serikali
kutokana na mfumo wa elimu wa sasa ni kwamba ukipanuwa wigo wa watu kupata
elimu kwamaana ya kujenga shule nyingi za msingi, shule nyingi za sekondari na
vyuo mbalimbali lazima uwe umeandaa fursa nyingi za ajira kama ajira
hazitapatikana na watu wanaamini wamesoma na wanastahili ajira, lakini kama serikali
haina mipango ya ajira kuna hatari ya watu hawa kuona serikali haina maana
kwasababu wao wanakuwa wanaamini kuwa wanayo elimu ya kutosha kuajiriwa kwanini
hawana ajira, matokeo yake ni kuzipinga serikali zilizoko madarakani,
tumeshuhudia makundi mengi Duniani yakipinga serikali zao makundi ya watu hao
wengi wao ni makundi ya watu waliosoma na kukosa ajira kwa hivi wanaona kama
serikali zao haziwajali kumbe elimu zao
haziwafanyi waweze kujitegemea.
Hasara kubwa ya kutaka kulazimisha kila
mtu aende sekondari ni kwamba ikitokea wakawa na uwezo wote wakuendelea na
masomo yao mpaka vyuo vikuu basi nchi hii itakuwa ni nchi ya mameneja na wakurugenzi
tu, kumbe ili nchi iendeshwe vizuri panatakiwa kuwe na watalaam wa kila aina na
hasa watalaam wa ngazi za chini na kuwa
na wachache wa ngazi za juu kwahiyo kwa mtazamo wangu ni kwamba tusiweke
matarajio yetu kuwaandaa vijana wa shule za msingi kuwa lazima waandaliwe
kwenda sekondari na katika hili niombe wizara ya Elimu chini ya waziri wake Ndugu
Ndalichako muone umuhimu wa kubadili umri wa watoto wa kuanza elimu ya msingi
badala ya umri wa miaka 6 au 7 basi umri usogezwe mpaka miaka 10 mtoto aanze
darasa la kwanza.
Maana yake ni nini hasa? Mkishakuwa na
elimu ya kujitegemea mtoto anapomaliza darasa la7 awe na uwezo wa kujitegemea
badala ya mfumo wa sasa ambapo mtoto anamaliza akiwa na mika 13 au 14 yaani
anafika kidato cha 4 ndo anakuwa na akili ya kukazana na masomo wakati muda
umepita.
Tusijilinganishe na watu wa mataifa ya
ulaya ambao mtoto wa miaka 14 ni mkubwa kiakili pamoja na kiumbo kutokana na
hali ya maisha walionayo sasa hapa unakuta kwasababu ya ugumu wa maisha mtoto
mwenye umri wa miaka 14 unaweza kudhani ana umri wa miaka 8 au 9 hili ni muhimu
sana tufanye mipango yetu ya elimu kama taifa kutokana na hali yetu sio kwakuwa
duniani huwa wanafanya hivi hapana.Hauwezi kuendesha maisha kwa kuiga maisha ya
jirani yako kwa kuwa anakula pilau kila siku na wewe unasema nami nakula pilau
kila siku bila ya kuangalia uwezo wako wa kula pilau ama Ugali wa Muhogo na
kisamvu.
Narudia tena kutokana na falsafa za
Plato watu wana vipaji mbalimbali, vipaji hivyo vinatakiwa kutambuliwa mapema
watoto wawapo shule za msingi na kuwabaini wale wanaostahili kuendela na masomo
ya sekondari na wale wasiostahili kutokana na uwezo wao wa kiakili wanapaswa
kupewa mafunzo ya stadi ili elimu hiyo iwafae kwa baadae.
Hivi mtu atakaesoma ufundi wa magari kwa
muda wa miaka 10 ni kimaanisha miaka 4 ya sekondari,miaka 2 ya kidato cha 5 na
6 na miaka 4 ya chuo kikuu badala ya kupita huko kote yeye miaka yote kumi
anasoma ufundi wa magari tu hivi hatuoni kuwa fundi huyu atakuwa injinia wa
hatari sana?Na kama serikali inafanya hivi inafanya kwa malengo, kwamba tutengeneze
mainjinia kadhaa wa kitu fulani kwa muda wa miaka kadhaa kwahiyo baada ya muda
fulani hamuezi kukosa wataalam katika taifa lakini tukiendelea kama
tunavyokwenda sasa ipo siku nchi hii itakosa wataalam kabisa na tukawa watu
wakwenda kuazima wataalam nje ambao tutakuwa tukiwalipa kiasi kikubwa cha pesa.
Duniani hakuna mtu aliezaliwa
mjinga kabisa labda awe ni mgojwa lakini vinginevyo kila mtu anawezakufanya
shughuli fulani na uwezo huo ni kutokana na uumbaji wa Mwenyezi Mungu katika kuhakikisha kuwa tunaishi kwa kutegemeana
kwamaana hiyo ni dhambi kubwa kumdharau yeyote kutokana na uwezo wake wa
kiakili na tukifanya hivyo tutakuwa tunamkosoa Mungu katika kazi yake kinachokushinda
wewe kinaweza kufanywa na yule,kama unajua hiki wenzako wanajua kile ndo maana
kuna Waalimu, Madaktari,Wanamichezo ambao nao wanatofautiana huyu mpira wa
miguu, yule anakimbia, na huyu kikapu, yule ngumi kwahiyo ni muhimu sana
kutengeneza elimu yenye kuwafaa watu badala ya kutengeneza elimu ambayo mwisho
wa siku baada ya watu kusoma wanarudi tena kuitazama serikali iwape ajira.
Kwahiyo
itakuwa ni miujiza na ndoto kuanza kuwaza juu ya kuanzisha viwanda huku hatuna
wataalam wa kuviendesha viwanda hivyo, natambua kuwa kwasasa zipo shule za
Ufundi lakini toka zijengwe na mkoloni mpaka leo shule hizo zimeendelea kuwa
mbovu kwa maana ya miundo mbinu na hii ni kumaanisha kuwa tangu nchi hii ipate
uhuru toka mwaka 1961 hatujaweza kujitegemea sawasawa maana kama shule
ilianchwa na mkoloni mapaka leo hakuna mabadiliko kuzidi yale ya mkoloni badala
yake tunarudi nyuma tutasema tumeweza kujitegeme?
Hili ni sawasawa na mtu anakupatia
Ngo’ombe 10 wa maziwa na kila Ng’ombe anazaa kwa mwaka mara moja inamaana kwa
mwaka mmoja unatakiwa kuwa na Ng’ombe 20 na
miaka mitano unatakiwa uwe na Ng’ombe 100 aliekupatia Ngo’ombe aliposafiri na kurudi baada ya miaka 5
alikuta una Ng’ombe wawili hivi
utahitaji tena upewe msaada au hao waliobakia wanapaswa kuchukuliwa?Maana pia
watapotea kwahiyo haiwezekani miaka zaidi ya 50 hatujafanya makubwa katika
shule hizi vinginevyo tuwe tumeanza kufikri kuwa na aina nyingine ya mfumo wa
elimu yetu lakini kama tunadhani shule hizi ni muhimu katika maendeleo ya nchi
na hasa nchi ya viwanda lazima hatua madhubuti zichukuliwe ili shule hizi ziwe
na hadhi yake ya zamani.
Mwisho nimalizie kwamba ni muhimu sana
kama taifa kuweka wazi aina ya mfumo wa maisha tunaotaka taifa letu liwe nao na
hili liwe jambo la kikatiba kwamba
pamoja na kwamba tuna mfumo wa vyama vingi lakini katiba iweke wazi kwamba
yeyote atakepewa dhama na wananchi kuiongoza Tanzaia lazima afuate sera na
mfumo tutakaokuwa tumekubaliana, kwahiyo mambo yote atakayokuwa anayafanya Rais
na serikali yake lazima yamlazimu kufuata mfumo huo na hii itarahisisha kupata
mfumo wa elimu tunaoutaka kwaajili ya Taifa.Pili hata kama serikali ingekuwa na
pesa nyingi kama mabomu ya Nyukilia ni vigumu sana kuwaajiri wananchi wake wote
njia bora ya kuwasaidia wananchi ni kuwapatia elimu ya kujitegemea.
Madhara ya elimu hii ya nadharia yameanza kuonekana,
kwanza watu maofisini waliowengi hawajui wanachokifanya.Yaani mtu anatoka chuo
kikuu utadhani sasa ndo ameingia darasani wakati yuko kazini, lakini pia lawama
zimeanza watu wakilia na serikali kuwa haiwapatii ajira hii yote ni kuwa na
mfumo wa elimu tegemezi hatutaweza kufanikiwa katika soko la ajira kama hatutabadili
mfumo wetu wa ajira.Haya hivi sasa tumekuwa kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki
kama nchi moja, wenzetu kwakuifahamu vema lugha ya kiingereza wanaonekana kuwa
wataalam zaidi kuliko sisi sasa tutashindanaje katika ajira?
Kama tunaona wenzetu wanatuzidi kwa sababu
ya lugha maana mifumo yao ya elimu pia inafanana na ya kwetu mfumo tegemezi ila
wao wanatuzidi kwasababu ya lugha, basi nasi tuamue kuwa lugha ya kufundishia
masomo yote toka shule ya msingi iwe kiingereza kwa hili pia hatueleweki wengine
wanasoma kiingereza wengine Kiswahili yaani utafikiri ni taifa moja lenye nchi
mbili.
Kwahiyo kabla ya kufikiri juu ya viwanda
tuanze na mfumo huu wa elimu, na jambo hili ni kubwa sana kwahiyo si lazima
likamilikekatika serikali hii iliyoko madarakani kwa sasa ni jambo la muda
mrefu kwahiyo pamoja na kwamba hatuna katiba mpya lakini ziwekwe kanuni ili
yeyote atakayechaguliwa kwa awamu zijazo aliendeleze sio kila mtu kuja na
utaratibu wake maana kipindi cha miaka 5 au 10 ya madaraka haitoshi kufanya
jambo kubwa namna hii japo awamu hii ya Mh
Rais John Pombe Joseph Maghufuli inawezakuanza, maana Dr Robert Schuller
katika kitabu chake cha hatua 26 za kuelekea kwenye mafanikio anasema Kuanza
jambo ni nusu ya kumaliza jambo hilo yaani(Beginning is Half done) kwahiyo
atakaekuja ataendelea kujenga juu ya msingi huo.
MAGABILO MASAMBU(29)
+255758379296,
+255717735023
Thanks alot Mr Mjalifu!
ReplyDelete