Awali ya
yote nawasalimia wazee wetu,salaam!
Ninayo
furaha kuandika waraka huu kwenu wazee wetu ambao kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu
mmeweza kuwepo mpaka leo toka mstaafu katika kuiongoza nchi yetu ya
Tanzania.Hongereni sana!
Lengo kuu la kuandika waraka huu kwenu ni
juu ya nia yangu ya dhati niliyonayo juu ya Taifa letu, kuona sisi kama Taifa
tunaendelea kuwa taifa la amani na ustawi katika kujiletea maendeleo
yaliyokusudiwa na mwasisi wa taifa hili Mwl J.K Nyerere baada wa ukombozi
kutoka mikononi mwa mkoloni.Na hii imetokana na mvutano uliopo sasa kati ya serikali
na vyama vya upinzani juu ya mikutano ya kisiasa.Pili nimeona nitumie nafasi
hii,kuweza kuwaomba ninyi kama walezi na wazee wetu wazoefu na nchi hii
kuingilia kati jambo kubwa namna hii ambalo linaweza kuiweka nchi mahali ambapo
sura yake ya zaidi ya miaka 50 ya uhuru itachafuka ndani ya muda mfupi, ndani
na nje ya nchi.Waswahili husema palipo na wazee huwa hapaharibiki jambo,na uzee
ni jalala ndiyo maana nawatupia jambo hili mlitazame kama wazee wazoefu na
siasa za nchi hii.
Kwanini
nimeandika waraka huu kwenu wala si kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania
ndugu Josephu John Pombe Magufuli,nimeandika kwenu kwa sababu moja tu kubwa
,kwakuwa mvutano huu unapande mbili hakika usuruhishi wake hauwezi kupatikana
miongoni mwa pande hizo mbili bali usuruhishi wake unapaswa kutoka kwa mtu wa
tatu ambaye atasikiliza maoni ya pande zote mbili,ili kujua nani yuko sahihi
kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,sina maana kuwa pande zote mbili
hazijui sheria bali kwakuwa zote zinavutana basi mvutano huo unaweza pia
ukaziba macho yao yasione nani mwenye haki kisheria.
Lakini pia
kwakuwa ninyi wazee wetu mpo bado angali hai,ni lazima tuwatumie wakati mwingine
kutatua mambo mazito kama haya,haiwezekani mambo yaharibike tuanze kuwalaumu
kwamba mpaka mambo yanaharibika hivi hawa
wazee
hawakuwapo? Na kwa jinsi hiyo pia tunakuwa tumetambua umuhimu wa uwepo wenu
kama walezi wa taifa.
Wako watu
katika taifa hili mimi nikiwa mmoja wapo ambao wanatamani uwepo wa wazazi wao
ili waweze angarau kuwashauri wanapokumbana na changamoto ngumu katika maisha,
lakini wazazi hao hawapo,sasa sisi kama taifa bado tunakila sababu ya kujivuna
kuwa na wazazi wetu ambao kazi kubwa iliyo baki kwenu nikutoa ushauri kwa
vijana wenu ili mambo yakae vema na heshima ya nchi yetu iendelee kutamalaki.
Tumesikia kauli mbali mbali zikitolewa pande
zote upande wa serikali na upande wa upinzani,kauli ambazo ukizipima
zinaashiria shari na sio amani,sasa sisi kama wananchi wa kawaida ambao
tumekulia katika nchi ya kistaarabu tunapata shida na kauli hizi kwamba malengo
yake ni nini,watanzania tunasifika duniani kwa uungwa,utu na ustaarabu wa hali
ya juu zaidi kauli hizi zinazotoka pande zote zinatufanya tupate shida ya
kutafsiri aina ya utu tulio nao leo,kwahiyo ndio maana nikaona niwaombe ninyi
wazee wetu mlitazame jambo hili kama linazungumzika.
Mfalme sulemani alimwomba Mungu ampatie mambo
mawili tu nayo ni Hekima na Busara,naamini mambo hayo mawili ninyi mnayo ndiyo
maana mliweza kuiongoza nchi hii na leo tunawaheshimu kama wazee wetu.Jambo
hili si la kukaa kimya,inawezekana hamjakaa kimya mmekuwa mkifanya juhudi za
kuhakikisha yale yanayotarajiwa kutokea yasitokee,lakini mimi kama kijana
ninayelitazama taifa hili kwa umri wangu sasa natimiza miaka 29 tangu
nijitambue skuwahi kuona kauli za namna hii ambazo zinatamkwa sasa.
Ndugu Jakaya
mrisho kikwete,mwaka jana nilikwandikia barua ya wazi iliyo toka katika gazeti
la Nipashe la tarehe 20 october 2015 ukurasa wa 7 yenye kichwa cha habari BARUA
YA WAZI WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA JK.
Barua hiyo
pia ilirudiwa katika gazeti la Mwanahalisi la tarehe 26,katika barua ile
nilionyesha wazi mambo makubwa na mazuri uliyoyafanya katika uongozi
wako,miongoni mwa hayo ilikuwa ni Jambo la barabara,Ujenzi wa shule za kata
ambazo kimsingi ndizo shule za kwanza kujengwa na serikali ya Tanzania na
mwisho nilieleza namna ambavyo ulikuza Demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na wananchi
wa nchi hii kuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza hilo nilikusifu sana na nikasema
utakapomaliza muda wako kama Rais wa Tanzania hautakuwa Rais mstaafu tu wa
Tanzania bali utakuwa kiongozi wa kimataifa na bado naamini ipo siku utakuwa
kiongozi mkubwa sana wa kimataifa.Hii ni kutokana na demokrasia uliyoijenga kwa kipindi
chako,inawezekana wapo watu walinishangaa kwa wakati huo lakini niliona dhamira
yako ya dhati ya kutohitaji kutenda maouvu juu ya wananchi wako.
Nichukue
nafasi hii tena nikuombe wewe pamoja na marais niliowataja hapo juu kulitazama
suala hili ambalo linatishia amani ya nchi yetu na mimi naamini siku zote meza
ya mazungumzo ndio huwa dawa katika migogoro yote,polisi,jeshi wala mahakama
huwa si suruhisho lenye kuleta mapatano bali mapatano ya kweli hupatikana
mezani ambapo pande mbili hukutanishwa na mtu wa tatu.
Tanzania ni nchi inayotazamwa na nchi karibu
zote Afrika na duniani kama mfano wa amani na uhuru wa watu wake,itakuwa aibu
kubwa nchi kuingia kwenye machafuko tufanane na majirani zetu najiuliza kama
tukiyaacha haya yakatimia ni nani atakuwa mshauri wa mwenzake? Ni waombe sana wazee
wetu bado sisi kama vijana tutapenda kuona tunaishi kwa amani, amani ambayo
itatokana na misingi ya Katiba na sheria za nchi tulizojiwekea.
Ningeamua
kunyamaza kimya lakini roho yangu hainitumi naona ninalo jambo la kuwaelezeni
ninyi ili kwa pamoja tuendelee kuifurahia nchi hii kama mlivyoweza kuifurahia
ninyi na leo mnaitwa viongozi wastaafu.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi
kusema maneno haya “Demokrasia
haiwezi kudumu ikiwa wachache hawatakubali matakwa ya wengi.Lakini matakwa ya
wengi hujurikana katika majadiliano au mazungumzo ya waziwazi. Kadhalika, matakwa
ya wachache hujulikana katika majadiliano na mazungumzo bila wale wachache
kusema waziwazi matakwa yao ,majadiliano hayana maana” Nyerere J.K (1962)
Tujisahihishe.
Hapa mwalimu
pamoja na mambo mengine msisitizo mkubwa hapa ni juu ya majadiliano ambayo
yanapaswa kutoka pande mbili ambazo zinavutana na ndiyo maana nikaona ni busara
mazungumzo hayo yawe na mtu wa tatu atakaye sikiliza hoja za pande zote na
kuhakikisha muafaka unapatikana na kila mtu analizika na uamzi wa majadiliano
hayo.
Mimi si
mwanasheria kwahiyo siwezi kusema nani mwenye haki kati ya serikali na vyama
vya upinzani,pia siwezi kusema nani asiye na haki katika kutekeleza shughuli
zake, wote wanaweza kuwa sahihi na wote wanaweza wasiwe sahihi lakini usahihi
huo ndio unapaswa kujengwa kwa hoja mbele yenu ili mfikie muafaka mzuri bila
kurushiana maneno,lazima tutambue kuwa sisi sote ni watanzania na nchi hii ni
ya kila mtu,akuna aliyemleta mwenzake duniani akamwambia wewe utaishi Tanzania
bali wote tumezaliwa katika ardhi hii ya Tanzania hivyo majadiliano mbele yenu
ni muhimu sana.
Silaha za
kivita marazote huwa hazileti amani,bali machafuko. Sisi wote ni mashuhuda wa
nchi ambazo wamekuwa katika migogoro ya kisiasa, lakini kinachowafikisha huko
nikutokuwepo majadiliano au mazungumzo yenye maelewano na athari zake si kwa
yule tu aliyekusudiwa hata yule aliyekusudia kufanya hivyo hupata athari,hivyo
kwa mtazamo wangu ni muhimu sana wazee wetu,viongozi wetu jambo hili mlitazame
kabla hatujashudia yale wengi wanaodhani yanaweza kutokea ili yaishe kwa amani
na tuendelee kuwa waalimu wa Amani Afrika na Duniani kote.
Mwisho,naamini bado sisi watanzania ni wamoja kwakuwa sisi sote ni ndugu na haya ndiyo
matunda aliyotuachia baba wa taifa letu Mwl J.K Nyerere hatubaguani kwa misingi
ya dini,kabila,rangi,au vyama vya siasa.Kama dalili za mambo haya zitaanza
kuonekana ni lazima tujiuleze ni kweli tutakuwa tunamuenzi mwl mtu ambaye
ametufanya leo tunajiona watanzania au tutakuwa wasalti wa fikra hizo?
Niwatakie
mafanikio mema katika mjadala huo ambao utatoa wingu zito lililotanda katika
anga la Tanzania huku tukiona maandalizi ya pande zote yakiendelea,
sijakamilika mtanisamehe pale nitakapokuwa nimewakwaza.
MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI
TANZANIA.
Magabilo
Masambu(29)
0758379296,0717735023.