Monday, 25 July 2016
Home »
» Fahamu historia ya Alexander Alexandrovich Prokhorenko shujaa kijana wa urusi wa mwaka 2016 katika mapigano ya Syria
Fahamu historia ya Alexander Alexandrovich Prokhorenko shujaa kijana wa urusi wa mwaka 2016 katika mapigano ya Syria
Alexander Alexandrovich Prokhorenko ni kijana mdogo aliyekuwa Komandoo katika Kikosi cha Kazi Maalum cha Jeshi la Urusi kiitwacho SPETSNAZ akiwa na cheo cha Luteni Mwandamizi (Senior Lieutenant). Alizaliwa tarehe 22 Juni 1990 katika kijiji cha Gorodki, Orenburg Oblast, nchini Urusi au Russia. Alihitimu masomo yake katika Skuli ya Uhandisi ya Ulinzi wa Makombora ya Ndege na katika Chuo cha Ulinzi wa Anga cha Smolensk nchini Urusi. Ndo kwanza alikuwa ameoa na mkewe alikuwa ndo kwanza anatarajiwa kujifungua muda si mrefu.
Alexander Alexandrovich Prokhorenko alikuwa miongoni mwa Makomandoo wa Kikosi cha Spetsnaz waliopelekwa nchini Syria kuisadia serikali ya Rais Bashar Al Assad katika mapigano dhidi ya kundi la ISIS. Alikuwa ni miongozi wa wanajeshi waliopelekwa kuuhami mji wa kihistoria wa Palmyira dhidi ya kundi hilo la ISIS.
Siku ya tarehe 17 Machi, 2016, kijana huyu akiwa katika jukumu lake zito la kukusanya taarifa muhimu za kijeshi zilizolenga kuwabaini wapiganaji wa ISIS mahali walipo na silaha zao na kisha kuzituma taarifa hizo kwa marubani wa ndege za kivita wa Urusi kwa ajili ya kuendesha mashambulizi ya anga yenye kupiga malengo vizuri, alijikuta amezingirwa na wapiganaji katili wa kundi la ISIS baada ya kumng'amua. Kama ilivyo mila na desturi kwa askari aliyefunzwa vyema na akafunzika, hasa komandoo, ni haramu na aibu kubwa kwa askari kuangukia mikononi mwa adui yake akiwa hai kwani anampa adui faida ya kumfanya atakavyo na kumsaidia kupata taarifa za jeshi lake iwapo atazidiwa na mateso atakayopewa na adui yake huyo.
Kwa kulielewa vyema hilo, Alexander Prokhorenko, baada ya kubaini kwamba alikuwa katikati ya wapiganaji wa kundi la ISIS na hakuwa na namna nyingine ya kufanya, aliamuru ashambuliwe kwa kombora na jeshi lake la anga na jeshi lilifanya hivyo mara moja na yeye kupoteza maisha akiwa kazini.
Kwa kushirikiana na vikosi vya Kikurd, jeshi la Urusi liliweza kuupata mwili wake na kuusafirisha kwenda Urusi ambapo uliwasili Moscow tarehe 29 Aprili, 2016. Mazishi yenye heshima zote yalifanyika nyumbani kwao katika kijiji cha Gorodki tarehe 6 Mei 2016. Tarehe 11 Aprili, 2016, Rais Vladimir Putin alimtangaza Alexander Prokhorenko kuwa Shujaa wa Shirikisho la Urusi, ambayo ni Heshima ya Juu zaidi nchini humo.
Huyu ndiye Alexander Alexandrovich Prokhorenko, ameacha mke mjazito. Pumzika kwa Amani Shujaa Kijana!!
0 comments:
Post a Comment