Taarifa Kuhusu Hali ya Uchumi wa Tanzania
Benki Kuu
ya Tanzania
Septemba 2016
YALIYOMO
Kwa
mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa, hali ya ukuaji wa uchumi wa
Tanzania imeendelea kuwa ya kuridhisha. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016,
ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5ikilinganishwa na
ongezeko la asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka 2015 (Kielelezo Na. 1).
Kielelezo Na. 1:
Mwenendo wa Ukuaji wa Uchumi Robo ya Kwanza ya Mwaka (Asilimia)
Chanzo:NBS, Ukokotoaji - Benki Kuu
Shughuli zilizochangia ukuaji huu wa uchumi kwa kiasi kikubwa ni pamoja na kilimo
(asilimia 11.7), biashara (asilimia 10.6), uchukuzi (asilimia 10.1), sekta ya
fedha (asilimia 10.1) na mawasiliano (asilimia 10.0).Shughuli za kiuchumi
zilizokua kwa kasi ya juu zaidi katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ni sekta ya
fedha (asilimia 13.5), mawasiliano (asilimia 13.4), na utawala wa umma
(asilimia 10.2) (Kielelezo Na. 2).
Kielelezo Na. 2a:
Ukuaji wa Shughuli Mbalimbali za UchumiRobo ya Kwanza ya Mwaka (Asilimia)
Kielelezo Na. 2b: Mchango wa Shughuli
Mbalimbali za Uchumikatika Ukuaji wa Uchumi Robo ya Kwanza ya Mwaka (Asilimia)
Kwa kuangalia viashiria mbalimbali inaonekana kuwa hali ya uchumi wetu itaendelea
kuimarika katika mwaka 2016. Kwa mfano:
Uzalishaji wa umeme nchini katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 umeongezeka kwa
asilimia 14.5 kufikia kWh milioni3,454.2 ikilinganishwa na kWh milioni3,016.7 katika
kipindi kama hicho mwaka 2015. Ongezeko hili limetokana kwa kiasi kikubwa na
jitihada za serikali katika kutumia nishati ya gesi kwenye uzalishaji umeme
kufuatia kukamilika kwa bomba la gesi kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam
pamoja na mtambo wa Kinyerezi I.Umeme unaozalishwa kwa kutumia nishati ya gesi
umeongezeka kwa asilimia 52.2(Kielelezo Na. 3). Hali hii itasaidia kuongezeka kwa uzalishaji viwandani
pamoja na sekta nyingine zinazotegemea nishati ya umeme, na hivyo kuchangia
katika kuongeza kwa pato la Taifa. Gharama
ya umeme itashuka pia.
Kielelezo Na. 3:
Mwenendo wa Uzalishaji Umeme Nchini
Januari - Juni
Uzalishaji wa saruji katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 umeongezeka kwa
asilimia 7 kufikia tani elfu 725.4 ikilinganishwa na tani elfu 680.1 zilizozalishwa
katika robo ya kwanza ya mwaka 2015. Hali hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na
ongezeko la uzalishaji wa kampuni ya Dangote ambayo ina uwezo wa kuzalisha tani
milioni tatu kwa mwaka(Kielelezo Na. 4).Ni matarajio yetu kwamba
uzalishaji katika kiwanda cha Dangote chenye uwezo wa tani milioni 3 na katika viwanda
vingine vya saruji nchini utaongezeka katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2016
kwani mahitaji ya nchi bado ni makubwa kuliko uzalishaji ulivyo hivi sasa.Aidha
kuna miradi mikubwa mingi ya hapo baadaye itakayokuwa na mahitaji makubwa ya saruji
kama vile mradi wa reli ya kati.
Kielelezo Na. 4:
Mwenendo wa Uzalishaji Sarujii
Januari – Machi
Uagizaji wa malighafi
za viwandanikutoka nje umeongezekakwa
asilimia 19.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 kufikia Dola za Marekani
milioni 520.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2015(Kielelezo
Na. 5). Hali hii imechangiwa na kuendelea
kukua kwa shughuli za uzalishaji viwandani. Ukuaji huu utaendelea kuchangia
pato la Taifa kiujumla katika mwaka 2016.
Kielelezo Na. 5:
Mwenendo wa Uagizaji Malighafi za Viwandani
Januari – Juni
Mauzo ya bidhaa za
viwanda nje ya nchi yameendelea kukua kwa kasi
ya kuridhisha. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 mauzo ya bidhaa nje ya nchi
yalifikia kiasi cha Dola za Marekani milioni 728.5, sawa na ongezeko la
asilimia 15.6 ikilinganishwa na kiasi kilichouzwa kipindi kama hicho mwaka 2015(Kielelezo
Na. 6).
Kielelezo Na. 6:
Mwenendo wa Uuzaji wa Bidhaa za Viwandani Nje ya Nchi
Januari – Juni
Makusanyo ya kodi katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 yameendelea kuwa
bora zaidi ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya mwaka 2015, ikiashiria kuimarika
kwa usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya serikali na kuendelea kuimarika kwa
hali ya
uchumi wa nchi.
Mikopo itolewayo na mabenki
ya biashara kwenye sekta binafsi,
imeendelea kuongezeka kwa kasi ya kuridhisha katika nusu ya kwanza ya mwaka
2016 kwa Shilingi bilioni 1,167.2, japo ni pungufu ikilinganishwa na ongezeko
la Shilingi bilioni 1,577.5 la mwaka 2015. Ongezeko hili linaendana na malengo
ya sera ya mwaka 2015/16 ambayo yanajumuisha utulivu wa mfumuko wa bei (Kielelezo
Na. 7).
Kielelezo Na. 7:
Mwenendo wa Ongezeko la Mikopo kwa Sekta Binafsi
Januari - Juni
Chanzo: Benki kuu
Miradi mikubwa ya
viwanda na miundombinu inayoendelea na inayotarijiwa kuanza kazi siku za usoni
itachangia katika kuimarisha uchumi. Hii ni pamoja na:
1. Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard gauge)
2. Ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda ambalo
litahusu vile vile upanuzi wa bandari ya
Tanga
3. Ujenzi wa Export Processing Zone ya Kurasini
– itakayokuwa mhimili wa biashara kati ya China na Ukanda huu wa Afrika
4. Mradi wa kuzalisha megawati 240 za umeme wa
Kinyerezi II unaoendelea kujengwa.
5. Miradi ya kupanua viwanja vya ndege nchini
kwa mfano- Dodoma, na mingine inayoendelea -katika viwanja vya Dar es Salaam,
Mwanza, Mbeya n.k.
6. Ujenzi wa maghala ya taifa ya kuhifadhi
chakula yenye uwezo wa kuhifadhi tani 350 yatakayojengwa kwa msaada wa Serikali
ya Hungary katika sehemu mbalimbali nchini hususan katika mikoa inayozalisha
mazao ya nafaka kwa wingi.
7. Kiwanda cha kuzalisha saruji cha Dangote
kilichopo Mtwara ambacho kipo mbioni kuzalisha kulingana na uwezo wake (full
capacity);
8. Kiwanda cha kutengeneza marumaru cha
Mkuranga, Pwani ambacho ujenzi wake unaendelea
9. Kiwanda cha kuzalisha mbolea mkoani Lindi -
kinajengwa
10. Kiwanda cha bidhaa za chuma – mkoani Pwani
ambacho kiko mbioni kukamilika.
Kwa kuzingatia mwenendo wa viashiria mbalimbali vya shughuli za uchumi, ni
dhahiri kwamba hali ya uchumi wa Tanzaniani nzuri na inatoa matumaini makubwa
kwamba shughuli halali za kiuchumi zinaendelea kutekelezwa kama ilivyotarajiwahapo
awalihivyo lengo la ukuaji wa pato la Taifa la asilimia 7.2 kwa mwaka 2016
litafanikiwa. Hii inachangiwa pia na ukweli kwamba serikali ya awamu ya tano imejipanga
katika kuimarisha uchumi endelevu usiokuwa na mianya ya rushwa;usimamizi thabiti
wa rasilimali za umma; na ujenzi wamiundombinu borakwa lengo la kujenga uchumi
wa viwanda chini ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
1.3 Mwenendo
wa Mfumuko wa bei
Wastani wa mfumuko wa bei katika
miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016 umeendelea kuwa mzuri ukiendelea kushuka
hadi kufikia asilimia 5.5 mwezi Juni 2016 na asilimia 4.9mwezi Agosti 2016
kutoka asilimia 6.8 mwezi Desemba 2015 (Kielelezo
Na. 8). Kushuka huku kwa wastani wa mfumuko wa bei kulichangiwa zaidi na
bei zisizojumuisha bei za vyakula na nishati (core inflation) zikifuatiwa na zile za nishati na mafuta.Wastani wa
mfumuko wa bei usiojumuisha bei za vyakula na nishati (core inflation), ambao ni kiashiria sahihi zaidi cha utekelezaji wa
sera ya fedha, umeendelea kubaki katika viwango vya chini (wastani wa asilimia
2.8 katika miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2016) kutokana na hatua mbalimbali thabiti
za sera ya fedha na bajeti katika kudhibiti ujazi wa fedha na ukwasi katika
uchumi.
Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea
kubakia katika viwango vya tarakimu moja katika siku zijazo na kufikia lengo la
muda wa kati la asilimia 5. Hii ni kutokana na matarajio ya hali nzuri ya hewa itakayochangia
kupungua kwa kasi ya kuongezeka kwa bei za vyakula, pamoja na ongezeko dogo la
bei ya mafuta nchini inayotokana na mwenendo wa bei ya mafuta katika soko la
dunia, na utulivu wa thamani ya Shilingi. Pia, mwendelezo wa sera thabiti ya
fedha, usimamizi mzuri wa matumizi na mapato ya Serikali, na upatikanaji wa
umeme utokanao na gesi ambao utasaidia kupunguza gharama za uzalishaji
viwandanivitaendelea kuimarishautulivu wa mfumuko wa bei. Hata hivyo ni muhimu
kuzingatia kuwa upungufu wa mavuno ya mazao ya chakula uliojitokeza kwa baadhi
ya nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika unaweza kusababisha shinikizo la mfumuko
wa bei katika siku za usoni.
Kielelezo Na. 8:
Mwenendo wa Mfumuko wa Bei (Badiliko la Miezi 12)
Chanzo:Benki kuu
Ili kufikia malengo ya serikali ya
kuimarisha uchumi na kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei, Benki Kuu imeendelea
kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti ukwasi ili uendane na mahitaji
halisi ya uchumi. Ongezeko la fedha taslimu (reserve money) ambacho ni kipimo cha ukwasi kwenye uchumi
limeendelea kubakia ndani ya malengo katika kipindi chote cha miezi sita ya
kwanza ya mwaka 2016. Katika kipindi hicho ujazi wa fedha taslimu ulikua kwa
wastani wa asilimia 11.6; wakati ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3)
ulikua kwa wastani wa asilimia 14.4, ikiwa ni ndani ya makadirio ya ukuaji
usiozidi asilimia 16.0 kwa mwaka 2015/16.
Wakati huohuo sekta ya fedha imeendelea kuchangia ukuaji wa
shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kasi nzuri ya kutoa mikopo kwa wakati na
kwa kiwango cha kutosha. Mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia
21.3 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016, sawa na kiwango kilichopatikana
katika kipindi kama hicho mwaka 2015. Mikopo mingi kwa sekta binafsi
ilielekezwa kwenye shughuli za biashara kwawastani wa asilimia 19.3 ya jumla ya
mikopo yote, shughuli za watu binafsi wastani wa asilimia 19.0, uzalishaji
viwandani wastani wa asilimia 10.6, uchukuzi na mawasiliano wastani wa asilimia
7.9, na shughuli za kilimo asilimia 7.8.
Benki Kuu inaendelea kutekeleza sera madhubuti ya fedha kwa kutumia
zana mbalimbali za sera ili kuhakikisha kwamba mahitaji ya ukwasi kwa ajili ya
shughuli mbalimbali za kiuchumi yanafikiwa bila ya kuchochea mfumuko wa bei.
Thamani ya Shilingi imeendelea
kuwa tulivu katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016, kufuatia hatua mbalimbali za
sera ya fedha zilizochukuliwa na Benki Kuu katika kusimamia hali ya ukwasi
kwenye uchumi pamoja na mwenendo wa uchumi ndani na nje ya nchi.Kuimarika kwa
sekta ya nje kulikotokana naongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi
na kupungua kwa thamani ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kumechangia katika
utulivu wa thamani ya shilingi. Kupungua kwa thamani ya bidhaa kutoka nje kumechangiwa
zaidi na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia. Katika kipindi cha
miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2016 Shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa kati
shilingi 2,180 hadi 2,190 kwa dola moja ya Marekani(Kielelezo Na. 9).
Kielelezo Na. 9: Mwenendo wa Thamani ya Shilingi
Chanzo:Benki kuu
Hali hii ya
utulivu wa thamani ya Shilingi kwenye soko huru la fedha inadhihirishakuwa sera
thabiti za uchumi pamoja na mwenendo mzuri wa urari wa mapato ya fedha za kigeni,
ndio jawabu la kulinda thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni na sio
kudhibiti matumizi ya dola kama ambayo imekuwa ikidaiwa mara kwa mara. Nchi
zenye udhibiti mkubwa wa fedha za kigeni mfano Afrika Kusini imeshuhudia
kuyumba sana kwa thamani ya fedha yake tofauti na shilingi ya Tanzania.
Hivyo nguvu
kubwa inapaswa ielekezwe katika kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta
mbalimbali hususan zile zinazoboresha urari wa malipo ya nje kama vile utalii,
viwanda, uchimbaji madini, kilimo n.k. Ikumbukwe kuwa uhuru wa kumiliki na
kutumia fedha za kigeni nchini Tanzania uliwekwa kama hatua ya kukabiliana na
hali iliyokuwepo miaka ya 1980 ya kuadimika sana kwa fedha za kigeni na mchango
wa uhuru huo tumeuona katika kuwepo kwa fedha za kigeni za kutosha. Nchi
zilizojaribu kuondoa uhuru huo, mfano Zambia, zimeshuhudia kutoweka kwa fedha
za kigeni kwenda nje. Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhimiza na kuweka
mazingira mazuri ya uzalishaji na kuondokana na fikra za kuingilia soko hurukama
jawabu la kulinda thamani ya shilingi.
Katika
miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016, sekta ya kibenki imeendelea kukua
ikichangiwa na uanzishwaji wa taasisi mpya za kifedha ikiwemo Benki ya Waalimu
Tanzania (Mwalimu Commercial Bank Plc) na Canara Bank (Tanzania) Limited.
Takwimu za awali za tathmini ya hali ya mabenki yetu zinaonesha kuwa mabenki
yetu ni imara na salama, yakiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha. Kufikia mwezi
Juni 2016, kulikuwa na jumla ya benki na taasisi za fedha zinazosimamiwa na
Benki Kuu zipatazo 65 zenye matawi 739 nchini kote.
Kiwango cha mitaji kikilinganishwa na mali iliyowekezwa (total
capital to total risk weighted assets and off-balance sheet exposures)
kilikuwa asilimia 17.17 kikilinganishwa na kiwango cha chini kinachotakiwa
kisheria cha asilimia 12.0. Hali ya ukwasi ambayo hupimwa kwa kuangalia uwiano
kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu na amana zinazoweza
kuhitajika katika muda mfupi (liquid assets to demand liabilities) ulikuwaasilimia
37.03 ukilinganishwa na uwiano wachini unaohitajika kisheria waasilimia 20(Jedwali Na. 1).
Amana za wateja katika mabenki zilipungua kutoka shilingi
trilioni 20.52 mwezi Desemba 2015 kufikia shilingi trilioni 20.24 mwezi June
2016. Miongoni mwa sababu zilizochangia kupungua kwa amana kwenye mabenki ni
pamoja na uamuzi wa Serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi na mashirika
ya umma kutoka mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania. Aidha mikopo (loans and overdafts) iliongezeka kutoka
shilingi trilioni 15.28 mwezi Desemba 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 15.67
mwezi Juni 2016.
Upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wasiofikiwa
na mabenki umeendelea kuongezeka kutokana na ubunifu wa mipango ya utoaji wa
huduma za malipo ya rejareja kupitia simu za mikononi, pamoja na huduma za
uwakala wa mabenki (agent banking services).
Kiujumla kwa
kuangalia viashiria vyote vya msingi hali ya ukwasi wa benki imeendelea kuwa ya
kuridhisha. Benki Kuu katika kusimamia majukumu yake ya kisera, imeendelea
kutoa mikopo ya muda mfupi kupitia “reverse
repos” pamoja na kununua fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya bidhaa
nje ya nchi kutoka kwenye benki. Kwa viashiria hivi ni dhahiri kwamba uamuzi wa
serikali wa kuagiza fedha zake zote kuwekwa kwenye akaunti maalum Benki Kuu
hakujasababisha sekta ya kibenki kutokuwa na ukwasi wa kutosha na kuacha
kukopesha kwa sekta binafsi kama inavyofikiriwa na baadhi yetu.
Ni vyema jamii ya
Watanzania ikafahamu kwamba akaunti ambazo fedha za mashirika zimehamishiwa
Benki Kuu ni akaunti za kukusanya mapato tu. Akaunti za matumizi bado ziko
katika benki za biashara ili kuyawezesha mashirika kufanya malipo kupitia
akaunti hizo. Hivyo, bado benki za biashara ni kiungo muhimu kati ya mashirika
ya umma na watoa huduma kwa mashirika hayo. Pia hali ya utoaji mikopo kama
tulivyoona awali ni nzuri na watanzania wanaendelea kuhudumiwa na benki zetu
kama inavyotarajiwa.
Jedwali Na. 1: Viashiria vya Uimara wa Sekta ya Fedha
Katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016, nakisi ya urari wa biashara ya
bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje (current account deficit) ilipungua kwa asilimia 61.7 na kufikia
nakisi ya dola za Kimarekani milioni 970.4, kutoka nakisi ya dola za Kimarekani
milioni 2,532.5 mwaka 2015. Kupungua huko kulitokana zaidi na ongezeko la
thamani ya bidhaa za viwandani, mapato yatokanayo na utalii na huduma za
usafirishaji nje ya nchi, pamoja na kupungua kwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa
kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za mitaji,na bidhaa za matumizi ya
kawaida.Katika kipindi cha miezi sita iliyoishia Juni 2016, kikilinganishwa na
kipindi kama hicho mwaka uliotangulia, thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa
nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 14.2 na kufikia dola za Kimarekani
milioni 4,473.2 wakati thamani ya bidhaa na huduma toka nje zilipungua kwa
asilimia 18.3 na kufikia dola za Kimarekani milioni 5,360.7
Hazina ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha na kuendelea
kukidhi mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza bidhaa na huduma nje
ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuongeza imani kwa wawekezaji katika uchumi wetu;
japo kumekuwepo na ucheleweshwaji wa fedha za wahisani na mikopo ya kibiashara
kutoka nje ya nchi. Hadi mwezi June 2016, akiba ya fedha za kigeni ilifikia
dola za Kimarekani milioni 3,870.3 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na
huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4. Wakati huo huo, rasilimali za
fedha za kigeni za mabenki (gross foreign
assets) zilikuwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 835.0
Deni la Taifa limeendelea kuongezeka na kufikia dola za Kimarekani milioni
20,851 mwishoni mwa mwezi Juni 2016, kutoka dola za Kimarekani milioni 19,861
mwezi Desemba 2015. Deni la nje liliongezeka kwa asilimia 2.6 na kufikia dola
za Kimarekani milioni 16,281 mwezi Juni 2016 (sawa na asilimia 77.8 ya deni la
taifa), kutoka dola za Kimarekani milioni 15,864 mwezi Desemba 2015.Hii
ilitokana na kuongezeka kwa mikopo mipya pamoja na malimbikizo ya malipo ya
madeni. Katika deni hilo la nje, asilimia 83.4 ni deni la Serikali na taasisi
za umma. Pamoja na ongezeko hilo, takwimu zinaonyesha kuwa deni letu bado ni
stahimilivu. Kwa mfano, deni la nje kwa thamani ya sasa (Net Present Value) ni karibu ya asilimia 20 ya Pato la Taifa,
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 50 ya Pato la Taifa (Sept-15 DSA). Hii
inaonyesha kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kukopa bila kuhatarisha ustahimilivu wa
deni letu.
Deni la ndani liliongezeka kufikia shilingi bilioni 10,038.4 mwishoni mwa
mwezi Juni 2016 kutoka shilingi bilioni 8,597.0 mwezi Desemba 2015. Ongezeko
hilo lilitokana na Serikali kukopa kupitia dhamana na hati fungani ajili ya
kugharamia bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, ikichangiwa pia na kupungua
kwa misaada na mikopo kutoka nje.
Jedwali Na 2 linaonyesha
vyanzo vya fedha za Serikali na matumizi yake katika kipindi cha miezi 6
kuanzia Januari hadi Juni 2016. Kama inavyoonekana jumla ya mapato ya ndani
ilikuwa shilingi bilioni 7,267 wakati matumizi ya kawaida (ukiondoa riba)
yalikuwa shilingi bilioni 6,488, hivyo mapato yalitosha kulipia matumizi ya
kawaida ya Serikali. Hii ni kuonyesha kwamba madeni ya nje na ndani yalitumika
kwa ajili ya miradi ya maendeleo pamoja na kurejesha madeni yaliyopita.
Jedwali Na. 2: Vyanzo vya Fedha vya
Serikali na Matumizi Yake (Shilingi bilioni)
|
Jan-16
|
Feb-16
|
Mar-16
|
Apr-16
|
May-16
|
Jun-16
|
Total
|
Total
resources
|
1,454.6
|
1,897.9
|
1,920.0
|
1,892.9
|
1,711.3
|
1,950.8
|
10,827.6
|
Domestic
revenue
|
1,151.2
|
1,079.6
|
1,325.5
|
1,083.5
|
1,086.3
|
1,541.1
|
7,267.2
|
Domestic
borrowing
|
210.0
|
687.5
|
433.3
|
718.0
|
320.8
|
180.8
|
2,550.3
|
Foreign
borrowing
|
64.4
|
87.9
|
146.7
|
72.6
|
287.7
|
219.9
|
879.1
|
Foreign
grants
|
29.0
|
43.1
|
14.6
|
18.8
|
16.5
|
8.9
|
130.9
|
Total
Uses
|
1,454.6
|
1,897.9
|
1,920.0
|
1,892.9
|
1,711.3
|
1,950.8
|
10,827.6
|
Recurrent
expenditure1
|
640.6
|
908.8
|
1,251.7
|
1,086.8
|
1,368.2
|
1,232.6
|
6,488.6
|
Domestic
debt service
|
419.5
|
407.6
|
422.3
|
241.0
|
179.5
|
482.9
|
2,152.9
|
Foreign
debt service
|
44.6
|
236.0
|
143.8
|
37.8
|
78.6
|
53.5
|
594.4
|
Development
expenditure
|
235.7
|
276.2
|
429.8
|
250.4
|
487.8
|
208.8
|
1,888.8
|
Adjustment
|
114.2
|
69.4
|
-327.7
|
276.8
|
-402.9
|
-27.0
|
-297.1
|
1Excluding interest payment
Chanzo: Wizara ya Fedha na Uchumi