Recent

JIFUNZE MAMBO MBALIMBALI YATAKAYOKUPA MAARIFA NA UJUZI MAISHANI

Saturday, 1 October 2016

WARAKA WANGU KWA (JPM)

WARAKA WANGU KWA (JPM)

Image result for magufuli picha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli


Na MAGABILO MASAMBU

Ndugu Mh. Rais,kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kukuandikia waraka huu,nitumie nafasi hii kukupongeza kwa kuchaguliwa na wananchi wa Tanzania katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015 oktoba na hatimaye ukawa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania hongera sana.


Pili nikupongeze kwa kuonyesha nia ya kutaka mabadiliko makubwa katika nchi yetu,kwa kutamani siku moja nchi yetu iweze kuwa nchi itakayojitegemea kiuchumi na mambo mengine kama hayo pia hongera.


Ndugu Mh.Rais ,waraka wangu kwako leo ni juu ya nia yako ya kutaka kuifanya Tanzania iwe nchi ya Viwanda kama msingi mkuu wa uchumi ambao tunafikiri kwa pamoja kwamba nia hiyo ikitimia basi itakuwa ni mkombozi wa Watanzania kujikwamua na jambo la Umaskini.


Pamoja na nia hiyo njema kuna maswali ambayo tunapaswa kuwa tumejiuliza kabla ya kutekeleza nia hiyo njema.Tukitazama historia ya nchi yetu tangu awamu ya kwanza jambo la viwanda ndilo hasa lilionekana kwamba lingewasaidia sana Wananchi wa Tanzania katika suala la uchumi,kwa kufahamu hilo Mwl J.K Nyerere Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadae Tanzania chini ya sera ya ujamaa alianzisha viwanda katika nchi yetu mfano Sungura,Mutex,Urafiki na vingine vingi.


Mwaka 1995 tulishuhudia sera ya ubinafsishaji,ambapo eti watu binafsi walionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuendesha viwanda na mashirika ya umma kwa faida kuliko serikali kwa hoja kwamba serikali inaendesha kwa hasara ama imeshindwa kujiendesha na hivyo watu waliojiita wawekezaji wakashika hatamu ya kuviendesha viwanda na mashirika hayo ya umma.


Ndugu Mh.Rais, maswali tunayopaswa kujiuliza kwa pamoja ni haya yafuatayo.Je,tutakapoanzisha viwanda leo tutachukua viwanda vyetu kutoka mikononi mwa wawekezaji hao? Je,tutawakaribisha wawekezaji wengine kama hawa walioko ndani ya nchi? Je,tutajenga viwanda vipya kabisa kutokana na fedha ya nchi yetu? Je kama tutajenga viwanda kwa fedha za mkopo tutazirudishaje?


Je kama tutajenga viwanda kwa fedha za misaada hao wanaotupatia misaada hiyo tutawalipa nini? Je,viwanda tulivyo navyo leo ambavyo viko mikononi mwa wawekezaji vimewasaidiaje watanzania? Kama havijawasaidia vya kutosha matatizo yanayofanya visiwasaidie Watanzania hawa kwa sasa yameshatatuliwa ili wawekezaji wengine kama hao wasifanye yaleyale wanayofanya hawa waliopo?


Hakika ndugu Mh.Rais tunapaswa kuwa tumejiuliza maswali mengi zaidi na kuyapatia majawabu kabla ya kuchukuwa hatua yoyote ya kuanzisha viwanda vipya.Mawazo na ushauri wangu kwako ni huu.Kwa kuwa tuna viwanda kwasasa ambavyo ni vya wawekezaji kama hao watakaokuja,wananchi wangehakikishiwa soko la uhakika katika viwanda hivi tulivyonavyo ili watakapokuwa wanalima mazao ambayo yanahitajika katika viwanda hivi kama malighafi waweze kuuza kwa faida.


Mfano wa kilimo cha miwa.Viwanda vya miwa tulivyonavyo walifika mahali wakawa wanahujumu juhudi za wakulima kwa kuwafanya wasiwe na uwezo wa kulima zao hilo na kuwauzia,ili viwanda vilime miwa yao kuepuka kununua miwa kutoka kwa wakulima,miwa mingi ya wakulima ilikuwa ikiozea mashambani baada ya kukatwa na kwa sababu wakulima walilima miwa hiyo kwa kutumia mikopo ilikuwa ni vigumu kwao kulima tena baada ya hujuma hizo.


Hii ni kwa sababu wawekezaji wengi wanakuwepo nchini kwaajili ya kutengeneza faida maradufu, hivyo wakaona ni vema walime miwa yao wenyewe kwa maana ya viwanda jambo ambalo lililazimu wananchi wa miwa kubadili mashambo yao na kuanza kulima mahindi na mpunga badala ya kilimo cha miwa.


Kwa hiyo upungufu wa Sukari pamoja na kwamba kumekuwepo na taarifa kwamba watu wanaficha Sukari, lakini mimi naamini hata kama ungewaambia wasage miwa yote iliyopo nchini bado sukari isingetosha kulisha nchi nzima, sababu ni hiyo kwamba kuna upungufu wa malighafi hiyo baada ya wakulima kuachana na kilimo hicho ambacho kumewafanya kuwa maskini zaidi.


Ndugu Mh.Rais naamini kwamba wakulima wa miwa na mazao mengine kama pamba,korosho,na kahawa ambayo yanahitajika katika viwanda vyetu wakihakikishiwa soko la uhakika wananchi hawa watalima kwa bidii na hiyo ndiyo njia pekee ya kumsaidia maskini wa Tanzania ili aweze kupata fedha inayotokana na jasho lake mwenyewe,sasa kama matatizo haya hayakuangaliwa basi hata viwanda vingine vikianzishwa vitakuwa na matatizo yaleyale ya miaka nenda rudi huku wananchi wakizidi kuteseka ndani ya nchi yao kana kwamba wameazimwa kutoka nchi jirani.


Ndugu Mh.Rais, unachopaswa kufahamu ni kwamba tangu utangaze kuwa Tanzania itakuwa nchi ya viwanda wananchi wengi hata kazi hawafanyi maana wamejawa matumaini makubwa kwamba neema inakuja wakati viwanda vilivyopo kwa kiasi kikubwa vimekuwa mateso kwao,mimi kama mwananchi wa kawaida najiuliza hivi hao wawekezaji watakaokuja watakuwa na tofauti gani na hawa waliopo kwasasa mpaka watu wawe na matumaini makubwa kiasi hikcho?


Ndugu Mh.Rais jambo la viwanda si jambo dogo na hasa katika nchi maskini kama zetu hizi ujenzi wake unahitaji muda,kwanza tupate wataalam katika ngazi zote maana haina maana tunakuwa na viwanda hapa halafu watendaji katika viwanda hivyo na hasa ngazi za juu ni wageni na watanzania wanabaki kuwa wabeba mizigo na wafagiaji.


Mimi ninavyolitazama jambo hili kwa muda wa miaka mitano au kumi bado nadhani ni muda mfupi sana kuwa na viwanda ambavyo vitaliacha Taifa likiwa salama katika uwanzishwaji wake kwa maana ya kuepuka mikopo na misaada ambayo inaweza kuwa tatizo kwa hapo baadaye.


Nia yako ni njema sana,hata watangulizi wako hawakuwa na nia mbaya katika kufikiri juu ya kuisaidia nchi tatizo huwa linakuja katika utekelezaji wa nia hiyo,na hasa suala la muda gani unataka jambo hilo liwe limekamilika,na kwa sababu wewe umesoma somo la Kemia unafahamu tofauti iliyopo kati ya Ugali unaopikiwa kwenye jiko la mkaa na ule unaopikiwa kwenye jiko la gesi!


Sina maana kwamba siwataki wawekezaji lakini pia lazima tujiulize ni kwa kiasi gani wawekezaji wamewasaidia wananchi zaidi ya kutengeneza faida kubwa na kuwafanya wananchi waendelee kuteseka.Mimi nadhani jambo hili kwa kiasi kikubwa tunapaswa kulifanya kwa kutumia fedha yetu ya ndani,tuweke mazingira rafiki ambayo hayataathiri nchi kwa wafanyabiashara wazalendo wa kitanzania 
pamoja na kutumia rasilimali zetu ambazo tunapaswa kuziuza kwa faida hata kama itatuchukuwa miaka 20 kukamilisha viwanda, lakini tuwe na utatuzi wa kudumu kuliko kulifanya jambo ili kwa haraka na tukajikuta tumeingia madeni na misaada itakayokuwa hatari kwa uhuru wa nchi yetu kutokana na masharti tutakayokuwa tukipewa.


Jambo kubwa hapa ni kuwatoa wananchi matumaini makubwa walionayo kwa sasa ili watambue kwamba hali ya nchi kiuchumi si nzuri kuliko wananchi kuendelea kuwa na matumaini makubwa ya muda mfupi.


Ndugu Mh.Rais katika malezi ya watoto nyumbani, siku zote watoto wanapaswa kufahamu hali halisi ya wazazi wao ili wawezekufanya juhudi za kutoka katika hali hiyo na anayetakiwa kuwafanya watoto wao waitambue hali ya wazazi wao si mtu mwingine bali ni wazazi wenyewe.


Kama viwanda vitaongezwa kwa wingi ndani ya muda mfupi naiona hatari ya viwanda hivyo kukosa malighafi za kutosha,kwa sababu mawazo ya watanzania wengi kwa sasa kila mtu anawaza nitafanya kazi kiwandani lakini hafikirii huko kiwandani tutakuwa tunafanya kazi kwa malighafi zipi pengine kama malighali itakuwa hewa ya Oksijeni ambayo imetapakaa kila mahali lakini kama malighafi hizo zitategemea uzalishaji wa watanzania lazima ziwepo juhudi za makusudi za kuhamasisha watanzania kujiandaa na uzalishaji huo kwa wingi.


Sina hakika kwamba kila mtu atafanya kazi ya umakenika,naamini lazima viwanda hivyo viwe na malighafi zinazotoka kwa wananchi wenyewe,sijaona kama kunajuhudi za kufikiri juu ya kuzipata.Wazazi wengi ambao huwa wanazaa watoto bila maandalizi tumeshuhudia wakiwatupa watoto wao lakini kwa mzazi aliye jiandaa kupata mtoto lazima anakuwa amefahamu pia matunzo ya mtoto huyo.


Mwisho,nikuombe ndugu Mh.Rais uweze kuyatafakari maswali niliyoyaweka hapo juu ili utakapotekeleza sera ya viwanda basi taifa letu libaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo ili tuendelee kuyafurahia  matunda ya nchi yetu kwa pamoja bila kujali misingi ya kikabila,kikanda,kidini au kivyama badala yake tutambue kwamba sisi ni wamoja kama taifa na kinachotutofautisha kati ya mtu na mtu ni tofauti za kimtazamo na kifikra ambazo  mimi naamini ni dalili nzuri za uhai wa Taifa.Tunapotofautiana kifikra inaonyesha ukomavu wa hali ya juu kwa watu wa Taifa hili,kwani watakuwa watetezi wa Taifa lao pale maadui watakapojaribu kutaka kuingilia uhuru wetu kama nchi.
                                                                                                                                                                                                                                 



 +255758379296
magabilomjalifu@yahoo.com

0 comments:

Post a Comment