WARAKA WANGU KWA (JPM)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk John Magufuli
Na MAGABILO MASAMBU
Ndugu
Mh. Rais,kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kukuandikia waraka huu,nitumie nafasi
hii kukupongeza kwa kuchaguliwa na wananchi wa Tanzania katika uchaguzi mkuu
uliofanyika mwaka 2015 oktoba na hatimaye ukawa Rais wa Jamhuri ya muungano wa
Tanzania hongera sana.
Pili
nikupongeze kwa kuonyesha nia ya kutaka mabadiliko makubwa katika nchi yetu,kwa
kutamani siku moja nchi yetu iweze kuwa nchi itakayojitegemea kiuchumi na mambo
mengine kama hayo pia hongera.
Ndugu
Mh.Rais ,waraka wangu kwako leo ni juu ya nia yako ya kutaka kuifanya Tanzania
iwe nchi ya Viwanda kama msingi mkuu
wa uchumi ambao tunafikiri kwa pamoja kwamba nia hiyo ikitimia basi itakuwa ni
mkombozi wa Watanzania kujikwamua na jambo la Umaskini.
Pamoja
na nia hiyo njema kuna maswali ambayo tunapaswa kuwa tumejiuliza kabla ya
kutekeleza nia hiyo njema.Tukitazama historia ya nchi yetu tangu awamu ya
kwanza jambo la viwanda ndilo hasa lilionekana kwamba lingewasaidia sana
Wananchi wa Tanzania katika suala la uchumi,kwa kufahamu hilo Mwl J.K Nyerere
Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadae Tanzania chini ya sera ya ujamaa
alianzisha viwanda katika nchi yetu mfano Sungura,Mutex,Urafiki na vingine vingi.
Mwaka
1995 tulishuhudia sera ya ubinafsishaji,ambapo eti watu binafsi walionekana
kuwa na uwezo mkubwa wa kuendesha viwanda na mashirika ya umma kwa faida kuliko
serikali kwa hoja kwamba serikali inaendesha kwa hasara ama imeshindwa
kujiendesha na hivyo watu waliojiita wawekezaji wakashika hatamu ya kuviendesha
viwanda na mashirika hayo ya umma.
Ndugu Mh.Rais, maswali tunayopaswa kujiuliza
kwa pamoja ni haya yafuatayo.Je,tutakapoanzisha viwanda leo tutachukua viwanda
vyetu kutoka mikononi mwa wawekezaji hao? Je,tutawakaribisha wawekezaji wengine
kama hawa walioko ndani ya nchi? Je,tutajenga viwanda vipya kabisa kutokana na
fedha ya nchi yetu? Je kama tutajenga viwanda kwa fedha za mkopo
tutazirudishaje?
Je
kama tutajenga viwanda kwa fedha za misaada hao wanaotupatia misaada hiyo tutawalipa
nini? Je,viwanda tulivyo navyo leo ambavyo viko mikononi mwa wawekezaji
vimewasaidiaje watanzania? Kama havijawasaidia vya kutosha matatizo yanayofanya
visiwasaidie Watanzania hawa kwa sasa yameshatatuliwa ili wawekezaji wengine
kama hao wasifanye yaleyale wanayofanya hawa waliopo?
Hakika
ndugu Mh.Rais tunapaswa kuwa tumejiuliza maswali mengi zaidi na kuyapatia
majawabu kabla ya kuchukuwa hatua yoyote ya kuanzisha viwanda vipya.Mawazo na
ushauri wangu kwako ni huu.Kwa kuwa tuna viwanda kwasasa ambavyo ni vya
wawekezaji kama hao watakaokuja,wananchi wangehakikishiwa soko la uhakika
katika viwanda hivi tulivyonavyo ili watakapokuwa wanalima mazao ambayo
yanahitajika katika viwanda hivi kama malighafi waweze kuuza kwa faida.
Mfano
wa kilimo cha miwa.Viwanda vya miwa tulivyonavyo walifika mahali wakawa
wanahujumu juhudi za wakulima kwa kuwafanya wasiwe na uwezo wa kulima zao hilo
na kuwauzia,ili viwanda vilime miwa yao kuepuka kununua miwa kutoka kwa
wakulima,miwa mingi ya wakulima ilikuwa ikiozea mashambani baada ya kukatwa na
kwa sababu wakulima walilima miwa hiyo kwa kutumia mikopo ilikuwa ni vigumu
kwao kulima tena baada ya hujuma hizo.
Hii
ni kwa sababu wawekezaji wengi wanakuwepo nchini kwaajili ya kutengeneza faida maradufu,
hivyo wakaona ni vema walime miwa yao wenyewe kwa maana ya viwanda jambo ambalo
lililazimu wananchi wa miwa kubadili mashambo yao na kuanza kulima mahindi na mpunga
badala ya kilimo cha miwa.
Kwa
hiyo upungufu wa Sukari pamoja na kwamba kumekuwepo na taarifa kwamba watu
wanaficha Sukari, lakini mimi naamini hata kama ungewaambia wasage miwa yote
iliyopo nchini bado sukari isingetosha kulisha nchi nzima, sababu ni hiyo
kwamba kuna upungufu wa malighafi hiyo baada ya wakulima kuachana na kilimo hicho
ambacho kumewafanya kuwa maskini zaidi.
Ndugu
Mh.Rais naamini kwamba wakulima wa miwa na mazao mengine kama pamba,korosho,na
kahawa ambayo yanahitajika katika viwanda vyetu wakihakikishiwa soko la uhakika
wananchi hawa watalima kwa bidii na hiyo ndiyo njia pekee ya kumsaidia maskini
wa Tanzania ili aweze kupata fedha inayotokana na jasho lake mwenyewe,sasa kama
matatizo haya hayakuangaliwa basi hata viwanda vingine vikianzishwa vitakuwa na
matatizo yaleyale ya miaka nenda rudi huku wananchi wakizidi kuteseka ndani ya
nchi yao kana kwamba wameazimwa kutoka nchi jirani.
Ndugu
Mh.Rais, unachopaswa kufahamu ni kwamba tangu utangaze kuwa Tanzania itakuwa
nchi ya viwanda wananchi wengi hata kazi hawafanyi maana wamejawa matumaini
makubwa kwamba neema inakuja wakati viwanda vilivyopo kwa kiasi kikubwa
vimekuwa mateso kwao,mimi kama mwananchi wa kawaida najiuliza hivi hao
wawekezaji watakaokuja watakuwa na tofauti gani na hawa waliopo kwasasa mpaka
watu wawe na matumaini makubwa kiasi hikcho?
Ndugu
Mh.Rais jambo la viwanda si jambo dogo na hasa katika nchi maskini kama zetu
hizi ujenzi wake unahitaji muda,kwanza tupate wataalam katika ngazi zote maana
haina maana tunakuwa na viwanda hapa halafu watendaji katika viwanda hivyo na
hasa ngazi za juu ni wageni na watanzania wanabaki kuwa wabeba mizigo na
wafagiaji.
Mimi
ninavyolitazama jambo hili kwa muda wa miaka mitano au kumi bado nadhani ni
muda mfupi sana kuwa na viwanda ambavyo vitaliacha Taifa likiwa salama katika
uwanzishwaji wake kwa maana ya kuepuka mikopo na misaada ambayo inaweza kuwa
tatizo kwa hapo baadaye.
Nia
yako ni njema sana,hata watangulizi wako hawakuwa na nia mbaya katika kufikiri
juu ya kuisaidia nchi tatizo huwa linakuja katika utekelezaji wa nia hiyo,na
hasa suala la muda gani unataka jambo hilo liwe limekamilika,na kwa sababu wewe
umesoma somo la Kemia unafahamu tofauti iliyopo kati ya Ugali unaopikiwa kwenye
jiko la mkaa na ule unaopikiwa kwenye jiko la gesi!
Sina
maana kwamba siwataki wawekezaji lakini pia lazima tujiulize ni kwa kiasi gani wawekezaji
wamewasaidia wananchi zaidi ya kutengeneza faida kubwa na kuwafanya wananchi
waendelee kuteseka.Mimi nadhani jambo hili kwa kiasi kikubwa tunapaswa
kulifanya kwa kutumia fedha yetu ya ndani,tuweke mazingira rafiki ambayo
hayataathiri nchi kwa wafanyabiashara wazalendo wa kitanzania
pamoja na kutumia
rasilimali zetu ambazo tunapaswa kuziuza kwa faida hata kama itatuchukuwa miaka
20 kukamilisha viwanda, lakini tuwe na utatuzi wa kudumu kuliko kulifanya jambo
ili kwa haraka na tukajikuta tumeingia madeni na misaada itakayokuwa hatari kwa
uhuru wa nchi yetu kutokana na masharti tutakayokuwa tukipewa.
Jambo
kubwa hapa ni kuwatoa wananchi matumaini makubwa walionayo kwa sasa ili
watambue kwamba hali ya nchi kiuchumi si nzuri kuliko wananchi kuendelea kuwa
na matumaini makubwa ya muda mfupi.
Ndugu
Mh.Rais katika malezi ya watoto nyumbani, siku zote watoto wanapaswa kufahamu
hali halisi ya wazazi wao ili wawezekufanya juhudi za kutoka katika hali hiyo
na anayetakiwa kuwafanya watoto wao waitambue hali ya wazazi wao si mtu
mwingine bali ni wazazi wenyewe.
Kama viwanda vitaongezwa kwa wingi ndani ya
muda mfupi naiona hatari ya viwanda hivyo kukosa malighafi za kutosha,kwa sababu
mawazo ya watanzania wengi kwa sasa kila mtu anawaza nitafanya kazi kiwandani
lakini hafikirii huko kiwandani tutakuwa tunafanya kazi kwa malighafi zipi
pengine kama malighali itakuwa hewa ya Oksijeni ambayo imetapakaa kila mahali
lakini kama malighafi hizo zitategemea uzalishaji wa watanzania lazima ziwepo
juhudi za makusudi za kuhamasisha watanzania kujiandaa na uzalishaji huo kwa
wingi.
Sina
hakika kwamba kila mtu atafanya kazi ya umakenika,naamini lazima viwanda hivyo viwe
na malighafi zinazotoka kwa wananchi wenyewe,sijaona kama kunajuhudi za
kufikiri juu ya kuzipata.Wazazi wengi ambao huwa wanazaa watoto bila maandalizi
tumeshuhudia wakiwatupa watoto wao lakini kwa mzazi aliye jiandaa kupata mtoto
lazima anakuwa amefahamu pia matunzo ya mtoto huyo.
Mwisho,nikuombe
ndugu Mh.Rais uweze kuyatafakari maswali niliyoyaweka hapo juu ili utakapotekeleza
sera ya viwanda basi taifa letu libaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo
ili tuendelee kuyafurahia matunda ya
nchi yetu kwa pamoja bila kujali misingi ya kikabila,kikanda,kidini au kivyama
badala yake tutambue kwamba sisi ni wamoja kama taifa na kinachotutofautisha
kati ya mtu na mtu ni tofauti za kimtazamo na kifikra ambazo mimi naamini ni dalili nzuri za uhai wa
Taifa.Tunapotofautiana kifikra inaonyesha ukomavu wa hali ya juu kwa watu wa
Taifa hili,kwani watakuwa watetezi wa Taifa lao pale maadui watakapojaribu
kutaka kuingilia uhuru wetu kama nchi.
+255758379296
magabilomjalifu@yahoo.com