Recent

MAARIFA YA MWENDOKASI

JIFUNZE MAMBO MBALIMBALI YATAKAYOKUPA MAARIFA NA UJUZI MAISHANI

Monday, 22 May 2017

Saturday, 11 February 2017

MAGABILO MASAMBU STAR TV NA MAADILI

Sunday, 18 December 2016

Je wajua! Ni biashara gani unapaswa kuzifanya mwaka 2017

1. Toa huduma.

Kama huna mtaji wa fedha, basi nina uhakika una mtaji wa muda. Sasa tumia muda wako kutoa huduma ambayo wengine wanaihitaji. Toa huduma kulingana na utaalamu wako, uzoefu wako au ujuzi ulionao. Angalia ni namna gani unaweza kutumia muda wako kuongeza thamani zaidi kwenye maisha ya wengine. Kwa mfano kama wewe ni mwalimu, basi unaweza kutenga muda wako wa ziada kutoa huduma ya kufundisha watoto shuleni au hata majumbani mwao. Kama wewe unaweza kufanya kitu fulani, basi tafuta wenye uhitaji wa kitu hiko na wasaidie kwa muda ulionao. Unaweza kuwasaidia watu kwa kazi zao za nguvu au hata kazi zao za kitaalamu. Unaweza kuwasaidia watu wanaofanya tafiti mbalimbali kwa muda wako na utaalamu wako kwenye tafiti. Kikubwa zaidi unaweza kutoa huduma ya ushauri kulingana na ujuzi na hata uzoefu ulionao kwenye maeneo mbalimbali. Iwe ni kilimo, biashara, afya na kadhalika.

2. Biashara ya mtandao (network marketing).

Najua wengi mkisikia hii huwa mnakunja sura na kuona kama mnapotezwa. Bado naendelea kusisitiza kama unataka kuigia kwenye biashara na hujui wapi uanzie, basi ingia kwenye biashara ya mtandao. Hii ni biashara ambapo unatumia bidhaa au huduma fulani, kisha unawashawishi wengine nao watumie na unalipwa kamisheni kwa manunuzi wanayofanya. Ni biashara nzuri kuingia kama hujawahi kufanya biashara kabisa na hujui wapi uanzie. Kwenye biashara hizi unafundishwa mengi na nyingi unaweza kuingia kwa mtaji kidogo wa chini ya shilingi laki moja.

3.Biashara ya taarifa na maarifa.

Unaweza kuingia kwenye biashara ya kutoa taarifa na maarifa. Kwa dunia ya sasa ambapo watu wengi wanatumia mtandao wa intaneti, unaweza kutumia mtandao huu kutoa taarifa na maarifa na kuweza kutengeneza kipato. Unaweza kufanya hivi kwa kuanzisha blog ambayo utaitumia kutoa taarifa na maarifa fulani ambayo wewe unayo, kwa ujuzi au uzoefu. Baadaye unaitumia blog hii kutengeneza kipato kwa kupitia matangazo na hata kuuza bidhaa na huduma zako nyingine. Pia unaweza kutoa taarifa na maarifa kwa njia ya uandishi wa vitabu. Unaweza kuandika vitabu na kuuza kwa nakala tete (softcopy) kama huna mtaji wa kuvichapa.

4. Kilimo biashara.

Kuna fursa kubwa sana kwenye kilimo cha kibiashara, hasa kwa kilimo cha muda mfupi cha mboga mboga na matunda. Kilimo hiki unaweza kuingia kwa mtaji kidogo na kama una muda wa kutosha kukifuatilia kwa makini basi unaweza kuanza kidogo na kukua kadiri muda unavyokwenda. Angalia kilimo kipi unaweza kuanza nacho na ukaribu wako ili uweze kupata matokeo mazuri.

5. Biashara yoyote unayotaka kuanza, ila anza kidogo.

Unaweza kuanza biashara yoyote unayopenda kuanza, hata kama ina uhitaji wa mtaji mkubwa, wewe anza kidogo. Anza kwa hatua ya chini kabisa, weka juhudi kubwa na endelea kuikuza. Ukishaanza kuona matokeo mazuri, yaani faida kwa hatua hiyo ndogo unayopiga, ni rahisi kuwakaribisha watu wengine na wakakuchangia mtaji. Au hata kwenda kwenye taasisi za kifedha na kuchukua mkopo. Wapo watu ambao wamekuwa wanafikiri kama wakipewa mkopo basi wataanzisha biashara, tatizo siyo mkopo, tatizo ni wewe kutojua biashara, ndiyo maana hakuna mtu mwenye akili zake timamu atakayekupa wewe mkopo wa kwenda kuanza biashara, kama hujawahi kufanya biashara kabisa. Kwa sababu anajua anakusindikiza kwenda kupata hasara. Anza biashara kidogo na ukishaanza kupata faida unaweza kuwashawishi watu wakupe mtaji zaidi.

Yangu ni hayo tu kwa.

Friday, 21 October 2016

CHADEMA: Kamati Kuu kukutana siku 2 kujadili hali ya siasa nchini

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Taarifa inatolewa kwa vyombo vya habari kuwa Kamati Kuu ya Chama itakutana kwa siku mbili, kuanzia Oktoba 22-23, mwaka huu, katika kikao chake cha kawaida. 

Kikao hicho kitakachofanyika jijini Dar es Salaam, pamoja na agenda mbalimbali, kitapokea na kujadili kwa kina taarifa ya hali ya siasa nchini na mwelekeo wa nchi kwa ujumla kiuchumi na kijamii.

Aidha, Kamati Kuu pia itapokea na kujadili taarifa ya fedha na Mpango wa Uchaguzi wa Kanda 10 za Chama, kabla ya Sekretarieti kuanza utekelezaji, ambao utahusisha kuwa na shughuli za chama, kisiasa na kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwatumikia wananchi, operesheni za uimarishaji wa chama nchi nzima na kuendelea kutoa elimu ya uraia. 

Imetolewa leo Ijumaa, Oktoba 21, 2016 na;

Tumaini Makene Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano CHADEMA

Tuesday, 11 October 2016

Zaidi ya Watanzania 450,000 wanaugua magonjwa ya akili


Watanzania wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha siku ya Afya ya Akili duniani huku Tanzania ikitajwa kuwepo kwa zaidi ya wagonjwa laki nne na nusu wanaougua maradhi hayo nchini. 
Aidha mkoa wa Dar es salaam ndio unaongoza kwa kuwa na wagonjwa ambapo sababu kubwa inatajwa kuwa ni matumizi ya kupindukia ya madawa ya kulevya ikiwa ni pamoja na Bangi. Kadhalika, mkoa wa Dodoma watu 12 wanapokelewa kila siku katika hospitali ya rufaa ya wagonjwa wa akili ya Mirembe kutokana na tatizo hilo. 

Maadhimisho hayo ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Dodoma katika hospitali ya taifa ya magonjwa ya akili Mirembe ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 10 ya mwezi wa kumi. Kauli mbiu ya maandimisho hayo ni “utu katika afya ya akili, huduma za kisaikolojia na afya ya akili kuwa huduma ya kwanza kwa wote” 

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mkuu wa wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme amewataka watanzania kuungana katika kupiga vita unyanyasaji na ukatili kwa wagonjwa wa akili na badala yake wapelekwe hospitali kwa ajili ya kupata matibabu. 

Amesema tatizo la akili huathiri kufikiri,kuhisi,kutambua na kutenda na tatizo la akili kwa sasa linaongezeka ambapo takribani watu milioni 35 wanaishi na ugonjwa huo.
Mkuu wa wilaya huyo amesema kwa mujibu wa taarifa ya akili na dawa za kulevya ya mwaka 2013/2014 za shirika la afya duniani(WHO)o mkoa unaoongoza kuwa na wagonjwa wengi ni Dar-es-salaam ambayo ina asilimia 2 ya wagonjwa ikifuatiwa na Mwanza yenye asilimia 1.2 huku mkoa wa mwisho ukiwa ni Rukwa wenye asilimia 0.2 

Naye Mganga mkuu wa Mkoa wa Dodoma, DK. James Kiologwe, amesema kwa mkoa wa Dodoma wagonjwa 1256 walipatikana katika kipindi cha mwaka 2015 na kila siku wanapokea wagonjwa 12 ambao wanaugua ugonjwa huo wa akili ambao wanatoka katika maeneo mbalimbali. 

Kwa upande wake, Mganga mkuu wa Hospitali ya rufaa ya wagonjwa wa akili Mirembe, Erasmus Mganga, ameeleza sababu kuu mbili zinazosababisha ugonjwa wa akili, kuwa ni ile ya mtu kuzaliwa na vinasaba vya ugonjwa huo ambapo vinakuwa ni vya kurithi na pia inatokana na magonjwa ambayo yanashambulia kwenye ubongo ambapo mtu anaweza kuugua ugonjwa wa Maralia, uti wa mgongo na mapafu ambapo huathiri ubongo. 

Amebainisha mgonjwa huyo akishatibiwa na kupona anabaki na tatizo kwenye ubongo na hivyo kupatwa na ugonjwa wa kichaa, kutokana na namna alivyoumwa.

Sunday, 2 October 2016

MECHI ZA YANGA vs SIMBA WANAMICHEZO NCHINI TUBADILIKE



Hapo jana katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kulikuwa na game kali ya watani wa jadi YANGA na SIMBA. Mechi hiyo ilikuwa na mvuto wa aina yake kwa pande zote mbili japo kulikuwa na changamoto mbili tatu ambazo zilitokea uwanjani lakini sio mbaya cha msingi ni kwamba mechi imekwisha na matokeo yameshapatikana.

Yapo mambo kadhaa ambayo yalitokea katika mchezo huo ambapo kimsingi wanamichezo tunapaswa kubadilika.

1. Ratiba ya mechi hiyo - Hapa wanaohusika ni TFF na bodi ya ligi, nimekuwa nikijiuliza kila siku hivi kwanini mechi ya Yanga na Simba huwa inapangwa siku ya peke yake? yaani kuna tatizo gani hasa endapo siku mechi hiyo inapochezwa pasiwepo mechi nyingine? Mbona katika ligi za wenzetu tunashuhudia mechi kali za dabi zinapochezwa siku hiyo hiyo kunakuwepo mechi nyingine? Nadhani kwenye hili tunapaswa kubadilika (Tusiishi kwa mazoea).

2. Vurugu kabla na baada ya mechi - Ni kweli kuwa mechi hii huwa na historia ya kipekee sana hapa nchini kwetu. Na inavuta hisia za mashabiki wengi wa soka hapa nchini. Lakini kitu cha kuzingatia hapa ni nidhamu ya mashabiki kabla na baada ya mechi hiyo. Kumekuwepo na mazoea mabaya ya washabiki kufanya vurugu wawapo nje ya uwanja na hata wakati mwengine ndani ya uwanja. Mi nadhani hili ni tatizo na wadau na mashabiki wa soka wanapaswa kubadilika na kuachana na vurugu bali washangilie kistaarabu bila ya kuhatarisha amani ya nchi.

3. Maamuzi ya refa uwanjani - Refarii ni miongoni mwa wanadamu waishio duniani, kama ni hivyo basi sifa kuu ya msingi ya kila binadamu ni UDHAFU (kutokukamilika). Katika mechi ya jana kulikuwa na makosa mawili yaliyofanya na refarii wa kati na moja ni mshika kibendera. Ni kweli kuwa Tambwe aliunawa mpira na ni kweli kuwa Ajibu/Mavugo hakuwa offside. Lakini makosa hayo ni ya kaida sana katika mchezo wa soka... Na refa anapotoa maamuzi ametoa. Sasa wewe ukifanya vurugu kwa kun`goa viti haisadii cha msingi ni kupeleka malalamiko baada ya mechi katika mamlaka zinazostahili.

Kwahiyo basi ni wakati wa kubadilika na kuachana na ushabiki usio wa maana. Tunatakiwa kuichukulia mechi hii kama ya kawaida kabisa. Haina haja ya kufanya mambo yasiyoeleweka wala presha kubwa....
         
.................WADAU WA SOKA TUBADILIKE..................

Saturday, 1 October 2016

WARAKA WANGU KWA (JPM)

WARAKA WANGU KWA (JPM)

Image result for magufuli picha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli


Na MAGABILO MASAMBU

Ndugu Mh. Rais,kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kukuandikia waraka huu,nitumie nafasi hii kukupongeza kwa kuchaguliwa na wananchi wa Tanzania katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015 oktoba na hatimaye ukawa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania hongera sana.


Pili nikupongeze kwa kuonyesha nia ya kutaka mabadiliko makubwa katika nchi yetu,kwa kutamani siku moja nchi yetu iweze kuwa nchi itakayojitegemea kiuchumi na mambo mengine kama hayo pia hongera.


Ndugu Mh.Rais ,waraka wangu kwako leo ni juu ya nia yako ya kutaka kuifanya Tanzania iwe nchi ya Viwanda kama msingi mkuu wa uchumi ambao tunafikiri kwa pamoja kwamba nia hiyo ikitimia basi itakuwa ni mkombozi wa Watanzania kujikwamua na jambo la Umaskini.


Pamoja na nia hiyo njema kuna maswali ambayo tunapaswa kuwa tumejiuliza kabla ya kutekeleza nia hiyo njema.Tukitazama historia ya nchi yetu tangu awamu ya kwanza jambo la viwanda ndilo hasa lilionekana kwamba lingewasaidia sana Wananchi wa Tanzania katika suala la uchumi,kwa kufahamu hilo Mwl J.K Nyerere Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadae Tanzania chini ya sera ya ujamaa alianzisha viwanda katika nchi yetu mfano Sungura,Mutex,Urafiki na vingine vingi.


Mwaka 1995 tulishuhudia sera ya ubinafsishaji,ambapo eti watu binafsi walionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuendesha viwanda na mashirika ya umma kwa faida kuliko serikali kwa hoja kwamba serikali inaendesha kwa hasara ama imeshindwa kujiendesha na hivyo watu waliojiita wawekezaji wakashika hatamu ya kuviendesha viwanda na mashirika hayo ya umma.


Ndugu Mh.Rais, maswali tunayopaswa kujiuliza kwa pamoja ni haya yafuatayo.Je,tutakapoanzisha viwanda leo tutachukua viwanda vyetu kutoka mikononi mwa wawekezaji hao? Je,tutawakaribisha wawekezaji wengine kama hawa walioko ndani ya nchi? Je,tutajenga viwanda vipya kabisa kutokana na fedha ya nchi yetu? Je kama tutajenga viwanda kwa fedha za mkopo tutazirudishaje?


Je kama tutajenga viwanda kwa fedha za misaada hao wanaotupatia misaada hiyo tutawalipa nini? Je,viwanda tulivyo navyo leo ambavyo viko mikononi mwa wawekezaji vimewasaidiaje watanzania? Kama havijawasaidia vya kutosha matatizo yanayofanya visiwasaidie Watanzania hawa kwa sasa yameshatatuliwa ili wawekezaji wengine kama hao wasifanye yaleyale wanayofanya hawa waliopo?


Hakika ndugu Mh.Rais tunapaswa kuwa tumejiuliza maswali mengi zaidi na kuyapatia majawabu kabla ya kuchukuwa hatua yoyote ya kuanzisha viwanda vipya.Mawazo na ushauri wangu kwako ni huu.Kwa kuwa tuna viwanda kwasasa ambavyo ni vya wawekezaji kama hao watakaokuja,wananchi wangehakikishiwa soko la uhakika katika viwanda hivi tulivyonavyo ili watakapokuwa wanalima mazao ambayo yanahitajika katika viwanda hivi kama malighafi waweze kuuza kwa faida.


Mfano wa kilimo cha miwa.Viwanda vya miwa tulivyonavyo walifika mahali wakawa wanahujumu juhudi za wakulima kwa kuwafanya wasiwe na uwezo wa kulima zao hilo na kuwauzia,ili viwanda vilime miwa yao kuepuka kununua miwa kutoka kwa wakulima,miwa mingi ya wakulima ilikuwa ikiozea mashambani baada ya kukatwa na kwa sababu wakulima walilima miwa hiyo kwa kutumia mikopo ilikuwa ni vigumu kwao kulima tena baada ya hujuma hizo.


Hii ni kwa sababu wawekezaji wengi wanakuwepo nchini kwaajili ya kutengeneza faida maradufu, hivyo wakaona ni vema walime miwa yao wenyewe kwa maana ya viwanda jambo ambalo lililazimu wananchi wa miwa kubadili mashambo yao na kuanza kulima mahindi na mpunga badala ya kilimo cha miwa.


Kwa hiyo upungufu wa Sukari pamoja na kwamba kumekuwepo na taarifa kwamba watu wanaficha Sukari, lakini mimi naamini hata kama ungewaambia wasage miwa yote iliyopo nchini bado sukari isingetosha kulisha nchi nzima, sababu ni hiyo kwamba kuna upungufu wa malighafi hiyo baada ya wakulima kuachana na kilimo hicho ambacho kumewafanya kuwa maskini zaidi.


Ndugu Mh.Rais naamini kwamba wakulima wa miwa na mazao mengine kama pamba,korosho,na kahawa ambayo yanahitajika katika viwanda vyetu wakihakikishiwa soko la uhakika wananchi hawa watalima kwa bidii na hiyo ndiyo njia pekee ya kumsaidia maskini wa Tanzania ili aweze kupata fedha inayotokana na jasho lake mwenyewe,sasa kama matatizo haya hayakuangaliwa basi hata viwanda vingine vikianzishwa vitakuwa na matatizo yaleyale ya miaka nenda rudi huku wananchi wakizidi kuteseka ndani ya nchi yao kana kwamba wameazimwa kutoka nchi jirani.


Ndugu Mh.Rais, unachopaswa kufahamu ni kwamba tangu utangaze kuwa Tanzania itakuwa nchi ya viwanda wananchi wengi hata kazi hawafanyi maana wamejawa matumaini makubwa kwamba neema inakuja wakati viwanda vilivyopo kwa kiasi kikubwa vimekuwa mateso kwao,mimi kama mwananchi wa kawaida najiuliza hivi hao wawekezaji watakaokuja watakuwa na tofauti gani na hawa waliopo kwasasa mpaka watu wawe na matumaini makubwa kiasi hikcho?


Ndugu Mh.Rais jambo la viwanda si jambo dogo na hasa katika nchi maskini kama zetu hizi ujenzi wake unahitaji muda,kwanza tupate wataalam katika ngazi zote maana haina maana tunakuwa na viwanda hapa halafu watendaji katika viwanda hivyo na hasa ngazi za juu ni wageni na watanzania wanabaki kuwa wabeba mizigo na wafagiaji.


Mimi ninavyolitazama jambo hili kwa muda wa miaka mitano au kumi bado nadhani ni muda mfupi sana kuwa na viwanda ambavyo vitaliacha Taifa likiwa salama katika uwanzishwaji wake kwa maana ya kuepuka mikopo na misaada ambayo inaweza kuwa tatizo kwa hapo baadaye.


Nia yako ni njema sana,hata watangulizi wako hawakuwa na nia mbaya katika kufikiri juu ya kuisaidia nchi tatizo huwa linakuja katika utekelezaji wa nia hiyo,na hasa suala la muda gani unataka jambo hilo liwe limekamilika,na kwa sababu wewe umesoma somo la Kemia unafahamu tofauti iliyopo kati ya Ugali unaopikiwa kwenye jiko la mkaa na ule unaopikiwa kwenye jiko la gesi!


Sina maana kwamba siwataki wawekezaji lakini pia lazima tujiulize ni kwa kiasi gani wawekezaji wamewasaidia wananchi zaidi ya kutengeneza faida kubwa na kuwafanya wananchi waendelee kuteseka.Mimi nadhani jambo hili kwa kiasi kikubwa tunapaswa kulifanya kwa kutumia fedha yetu ya ndani,tuweke mazingira rafiki ambayo hayataathiri nchi kwa wafanyabiashara wazalendo wa kitanzania 
pamoja na kutumia rasilimali zetu ambazo tunapaswa kuziuza kwa faida hata kama itatuchukuwa miaka 20 kukamilisha viwanda, lakini tuwe na utatuzi wa kudumu kuliko kulifanya jambo ili kwa haraka na tukajikuta tumeingia madeni na misaada itakayokuwa hatari kwa uhuru wa nchi yetu kutokana na masharti tutakayokuwa tukipewa.


Jambo kubwa hapa ni kuwatoa wananchi matumaini makubwa walionayo kwa sasa ili watambue kwamba hali ya nchi kiuchumi si nzuri kuliko wananchi kuendelea kuwa na matumaini makubwa ya muda mfupi.


Ndugu Mh.Rais katika malezi ya watoto nyumbani, siku zote watoto wanapaswa kufahamu hali halisi ya wazazi wao ili wawezekufanya juhudi za kutoka katika hali hiyo na anayetakiwa kuwafanya watoto wao waitambue hali ya wazazi wao si mtu mwingine bali ni wazazi wenyewe.


Kama viwanda vitaongezwa kwa wingi ndani ya muda mfupi naiona hatari ya viwanda hivyo kukosa malighafi za kutosha,kwa sababu mawazo ya watanzania wengi kwa sasa kila mtu anawaza nitafanya kazi kiwandani lakini hafikirii huko kiwandani tutakuwa tunafanya kazi kwa malighafi zipi pengine kama malighali itakuwa hewa ya Oksijeni ambayo imetapakaa kila mahali lakini kama malighafi hizo zitategemea uzalishaji wa watanzania lazima ziwepo juhudi za makusudi za kuhamasisha watanzania kujiandaa na uzalishaji huo kwa wingi.


Sina hakika kwamba kila mtu atafanya kazi ya umakenika,naamini lazima viwanda hivyo viwe na malighafi zinazotoka kwa wananchi wenyewe,sijaona kama kunajuhudi za kufikiri juu ya kuzipata.Wazazi wengi ambao huwa wanazaa watoto bila maandalizi tumeshuhudia wakiwatupa watoto wao lakini kwa mzazi aliye jiandaa kupata mtoto lazima anakuwa amefahamu pia matunzo ya mtoto huyo.


Mwisho,nikuombe ndugu Mh.Rais uweze kuyatafakari maswali niliyoyaweka hapo juu ili utakapotekeleza sera ya viwanda basi taifa letu libaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo ili tuendelee kuyafurahia  matunda ya nchi yetu kwa pamoja bila kujali misingi ya kikabila,kikanda,kidini au kivyama badala yake tutambue kwamba sisi ni wamoja kama taifa na kinachotutofautisha kati ya mtu na mtu ni tofauti za kimtazamo na kifikra ambazo  mimi naamini ni dalili nzuri za uhai wa Taifa.Tunapotofautiana kifikra inaonyesha ukomavu wa hali ya juu kwa watu wa Taifa hili,kwani watakuwa watetezi wa Taifa lao pale maadui watakapojaribu kutaka kuingilia uhuru wetu kama nchi.
                                                                                                                                                                                                                                 



 +255758379296
magabilomjalifu@yahoo.com